Serikali yavuka lengo sensa ya watu na makazi

Anna Makinda

SERIKALI imevuka lengo katika siku ya kwanza ya sensa ya watu na makazi kwa kuhesabu watu 10,259,497 badala ya watu milioni 10 waliolengwa awali.

Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) jumatano ilisema ongezeko hilo ni sawa na asilimia 0.45 hivyo badala ya kufikia asilimia 15 tu, asilimia 15.45 ilifikiwa.

Mratibu wa Sensa Taifa NBS, Seif Kuchengo alisema katika siku hiyo ya kwanza makarani walikusanya taarifa katika kaya 2,346,599 kote nchini.

Advertisement

Kuchengo alisema katika siku ya kwanza makarani walihesabu wanawake 5,305,533 sawa na asilimia 51.7 na wanaume 4,953,964 sawa na asilimia 48.3.

HabariLEO jumatano lilishuhudia takwimu za idadi ya watu, kaya kwa jinsi na umri zikiingia moja kwa moja kwenye ukurasa wa kupokea matokeo kwenye kituo cha kupokea NBS kutoka kwenye vishikwambi.

Hadi jumatano jioni Mtwara ilihesabu asilimia 21, Ruvuma asilimia 20, Njombe asilimia 21 na Iringa asilimia 20.9 na Mkoa wa Dodoma ulihesabu asilimia 15.41.

Katika kuhoji wanakaya wengi zaidi, Mkoa wa Dar es Salaam iliongoza, ukifuatiwa na Mwanza na Shinyanga.

Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi, Anne Makinda jana alisema sensa inaendelea kama ilivyopangwa na hadi jumatano asubuhi ukusanyaji wa taarifa ulifikia asilimia 17.13 ya kaya milioni 14 zilizopo nchini.

Makinda aliwaeleza waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuwa kituo cha kuchakata taarifa za sensa kipo jijini Dodoma na kwamba wana imani kasi ya ukusanyaji kwa siku zilizobaki itaendelea kuwa kubwa zaidi.

Alisema karani wa sensa atapita katika kaya kuweka miadi na mkuu wa kaya na kuacha fomu ambayo mkuu wa kaya atajaza taarifa muhimu za watu wote waliolala katika kaya yake usiku wa kuamkia Agosti 23 mwaka huu.

Makinda aliagiza waratibu wa sensa wa mikoa na wilaya wahakikishe fomu zinasambazwa katika kaya kuharakisha kazi hiyo na ifahamike kuwa makarani wa sensa wamejiandaa kufanya kazi asubuhi kabisa kabla mkuu wa kaya hajaondoka kwenda kazini na jioni baada ya mkuu wa kaya kurudi nyumbani.

Pia aliagiza waratibu wa sensa wa mikoa na wilaya waandae utaratibu wa kuwa na namba ya simu ambayo wananchi wataitumia kupiga simu kama watakuwa bado hawajahesabiwa baada ya tarehe 29 Agosti mwaka huu.

Makinda alisema makarani waliopoteza vishikwambi malipo yao ya mwisho yatasimamishwa.