Serikali Zanzibar yaanzisha kituo elimu mjumuisho
ZANZIBAR, Serikali ya Zanzibar imeendelea kuweka kipaumbele kwa watu wenye ulemavu kwa kuweka msisitizo katika kuboresha mazingira ya elimu kwa kuanzisha Kituo cha Elimu Mjumuisho Pujini, Wilaya ya Chakechake Pemba.
Makamu wa Pili wa Rais, Hemed Suleiman Abdulla, alifungua rasmi kituo hicho ikiwa ni muendelezo wa shamrashamra za kutimiza Miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Akieleza kuwa serikali inatekeleza mipango ya kitaifa na kimataifa ya kuhakikisha shule za elimu mjumuisho zinatoa huduma bora, zikiwawezesha wanafunzi wenye mahitaji maalumu kupata elimu ili kujenga mustakabali wao.
Kituo hicho ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa maendeleo wa Zanzibar (ZAPED 2021-2026) na malengo ya maendeleo endelevu ya Dunia (SDG 2030). Hivyo, serikali inaonyesha dhamira yake ya kutoa fursa sawa za elimu kwa wote, ikijumuisha kikamilifu wanafunzi wenye ulemavu.
Hata hivyo hatua hii inaendana na malengo ya waasisi wa mapinduzi matukufu ya mwaka 1964 ya kutoa elimu bora kwa wananchi wote bila ubaguzi.