WAKUSANYAJI mapato katika mamlaka 98 za serikali za mitaa hawakuwasilisha Sh bilioni 11.07 katika akaunti husika za benki. Hii ni kwa mujibu wa ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere.
Amezungumza hayo leo Machi 29, 2023 Ikulu Magogoni, Dar es Salaam, wakati akitoa taarifa kuhusu uwasilishaji wa ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2022.
Akiwasilisha ripoti hiyo, CAG Charles Kichere amesema suala hilo limetokana na ufuatiliaji duni na kutofanya upatanisho wa hesabu za mara kwa mara.
Ripoti hiyo imeeleza kuwa wakala wa ukusanyaji wa mapato katika mamlaka 10 za serikali za mitaa, hawakuwasilisha Sh bilioni 4.12 kwenye benki.
Aidha, CAG Charles Kichere amewashauri wakurugenzi wa mamlaka za serikali za mitaa kuhakikisha fedha zote ambazo hazikuwekwa benki zinawekwa kwa kufuata sheria za ukusanyaji wa mapato ya serikali.