Sh bilioni 11 kupunguza vifo vya wajawazito na watoto MNH

DAR ES SALAAM: SERIKALI chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imewekeza zaidi ya Sh bilioni 11 katika sekta ya afya hususani katika huduma za mama na mtoto.
Lengo la uwekezaji huo ni kupunguza vifo vitokananavyo na uzazi na kuhakikisha kuwa kila mtanzania anayezaliwa anakuwa salama.
Hayo yamesemwa leo Januari 27, 2024 na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo katika zoezi la kufanya usafi na kupanda miti katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ikiwa ni kusherehekea siku ya kuzaliwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan.
Mpogolo amesema kuwa Hospitali ya Taifa Muhimbili ni kimbilio kwa kila Mtanzania na kwa kutambua hilo Rais Samia amewekeza vifaa tiba vya ambavyo vitaweza kumsaidia mama na mtoto anayekuja Muhimbili kupata huduma.
“Kwa kutambua umuhimu wa afya ya Watanzania Rais amewekeza vifaa tiba hapa vya takribani Sh bilioni 11 pia amechangia fedha zake binafsi kiasi cha Sh bilioni 1 kwa ajili ya kuboresha huduma ya mama na mtoto na haya yote amefanya kwa dhati kabisa ili kumlinda mama na mtoto anayezaliwa,” amesema Mpogolo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili ,Prof Mohamed Janabi amewataka watanzania kutumia uwekezeji huo uliofanywa na Serikali katika kufanya uchunguzi wa afya zao kabla ya kuugua.
“Gharama za matibabu ni ghali hivyo ni vyema mkajenga tabia ya kufanya uchunguzi wa afya kwa kuwa kinga ni bora kuliko tiba, njooni mfanye uchunguzi wa afya zenu”amesema Prof. Janabi
Aidha, amewasisitiza wananchi kujitokeza kufanya uchunguzi wa saratani ikiwemo saratani ya matiti na mlango wa kizazi kwa wanawake na saratani ya tezi dume kwa wanaume kwa kuwa saratani ikigundulika mapema inaweza kutibika na mtu akapona kabisa.



