Sh bilioni 5.8 kubadili sura utoaji huduma Hanang

MANYARA: Serikali ya Awamu ya Sita imewekeza zaidi ya Sh bilioni 5.8 katika ujenzi wa Jengo la Utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Hanang’, mkoani Manyara mradi unaotarajiwa kuleta mapinduzi makubwa katika utoaji wa huduma kwa wananchi wa wilaya hiyo.
Hayo yamebainishwa leo Juni Mosi, 2026 Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Kenani Kihongosi alipotembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa jengo hilo ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya kikazi mikoa ya Kaskazini.

Awali taarifa ya mradi iliyoendaliwa na Mkuu wa Wilaya ya Hanang’,Almish Hazali ilieleza kuwa fedha za mradi huo zilitolewa katika mwaka wa fedha 2025/2026 na hadi sasa umefikia asilimia 35 ya utekelezaji wake.
Amesema kuwa mradi huo unaotekelezwa katika mji wa Katesh unalenga kuweka ofisi za kisasa zitakazorahisisha upatikanaji wa huduma za serikali katika eneo hilo.
Akizungumza baada ya kupikea taarifa hiyo Kihongosi ameelekeza mradi ukamilike kwa wakati na ujengwe kwa kuzingatia ubora ambao utaendana na fedha zilizotolewa kwa ajili ya utekelezaji.

Pia amesema kuwa hataki kusikia manung’uniko juu ya malipo ya vibarua wanaofanya kazi katika mradi huo, akisisitiza kuwa waliowe stahiki zao kwa wakati ili waweze kunufaika na miradi inayopelekwa na serikali.



