Sh bilioni 83 zatengwa ujenzi mabwawa, skimu za umwagiliaji

NAIBU Waziri wa Kilimo, Anthony Mavunde leo Januari 18, 2022 ametembelea Bwawa la Kata ya Igurusi na skimu ya umwagiliaji ya Igumbuilo wilayani Mbarali mkoani Mbeya ikiwa ni mkakati wa hatua za awali za serikali kuanza ujenzi ambapo imetenga Shilingi bilioni 83

Akizungumza na HabariLeo, Mavunde amesema serikali imepanga kuendeleza ekari 91, 231 zitakazotumiwa na wakulima kuzalisha mazao yenye tija.

Amesema, hatua hiyo ni maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuboresha Mpaka wa GN. 28.

“Sisi kama Serikali tumejipanga kuhakikisha kwamba tunajenga miundombinu rafiki ambayo haitaruhusu upotevu wa maji, kumfanya mkulima azalishe mwaka mzima kwa tija na baadae maji yatakayotumika yaweze kutiririka kwenda Mto Ruaha kwa ajili ya shughuli nyingine za kimaendeleo.”Amesema

Amesema kukamilika kwa ujenzi wa miradi hiyo Mbarali kutaenda sambamba na kuwapanga wakulima kwenye mashamba ikiwa ni pamoja na kuimarisha huduma za ugani, ili wazalishe kwa tija zaidi na kujiongezea kipato.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Raymond Mndolwa alieleza kuwa Serikali katika bajeti ya mwaka 2022/2023 imetenga zaidi ya bilioni 83 kwa ajili ya kuendeleza miundombinu ya umwagiliaji wilayani Mbarali ikiwemo ujenzi wa mabwawa na skimu za kisasa na kwamba katika mwaka ujao wa fedha 2023/24 serikali itaanza utekelezaji wa miradi hiyo.

Wakati huohuo, Mbunge wa Jimbo la Mbarali, Francis Mtega aliishukuru Serikali kwa kuleta miradi mikubwa ya umwagiliaji wilayani Mbarali ambayo inalenga kuwaongezea kipato wana Mbarali na kuchangia zaidi kwenye upatikanaji wa chakula nchini.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Reuben Mfune alimueleza Naibu Waziri Mavunde kuwa, kilio kikubwa cha wananchi wa Mbarali kimesikika kuhusu kuendeleza skimu za wakulima wadogo zipatazo 88 ili waweze kuzalisha kwa tija.

Habari Zifananazo

Back to top button