Shule Kibaha wahamasisha jamii ujenzi wa madarasa
PWANI; Kibaha. SHULE ya msingi Kambarage, iliyopo Halmashauri ya Kibaha,mkoani Pwani inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa madarasa, hali inayosababisha mrundikano wa wanafunzi wakati wa masomo katika darasa moja
Akitoa taarifa ya shule hiyo wakati wa habarambee ya kuchangisha fedha za ujenzi wa madarasa nane na matundu ya vyoo, Mkuu wa shule ya msingi Kambarage, Happy Msaki, amesema wanaupungufu wa madarasa nane na matundu ya vyoo 26.
Alisema shule hiyo ambayo ina zaidi ya wanafunzi 800 ina upungufu mkubwa wa madarasa hali ambayo imechangia mrundikano wa wanafunzi katika darasa moja na kwamba jumla ya Sh milioni 197 zinahitajika kukamilisha ujenzi wa madarasa hayo.
“Shule yetu ina jumla ya wanafunzi 878, madarasa tulionayo hayatoshelezi mahitaji wanafunzi wanasoma kwa shida kutokana na kuwa wengi katika darasa moja ..yapo baadhi ya madarasa ambayo tumeanza ujenzi ambayo hayajakamilika kutokana na ukosefu wa fedha,”alisema
“Kufanyika kwa harambee hii imetusaidia kupata fedha za kumalizia madarasa yetu na matundu ya vyoo, Ila pia niombe wadau wengine mbalimbali waendelee kuichangia shule yetu ili lengo la serikali la kutoa elimu bora lifanikiwe,”alisema
Mgeni rasmi katika harambee hiyo ambaye ni mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSSF), Heri Kasingo, alisema taasisi hiyo imetoa Sh milioni mbili kuchangia ujenzi wa madarasa hayo na kwamba ni wajibu wa jamii kuchangia shughuli mbalimbali za kimaendeleo.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Nickson John, alikiri kuwepo upungufu wa madarasa katika baadhi ya shule wilayani humo, ikiwemo shule hiyo na kwamba changamoto hiyo inatokana na ongezeko kubwa la wanafunzi katika msimu wa uandikishaji.
“Upungufu wa madarasa upo kwa baadhi ya shule katika wilaya yangu na sababu ipo wazi kutokana na ongezeko la wanafunzi, ila serikali chini ya Rais Samia Hassan Suluhu, bado imeendelea kufanya kazi kubwa za maendeleo, ambapo kwa mwaka huu shule nne mpya zimejengwa za msingi mbili na sekondari mbili,”alisema.