Sido washauriwa kushirikiana na TBS ubora wa bidhaa

SHIRIKA la kuhudumia viwanda vidogo(Sido) Mkoa wa  Dodoma limeshauriwa kushirikiana na Shirika la Viwango( TBS), ili kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa na vijana zinakuwa na ubora.

Kauli hiyo imetolewa na Mkurugezi wa Idara ya Ukuzaji  Ajira na Ujuzi  kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ally Msaki kwenye hafla ya kuhitimisha mafunzo ya uanagenzi kwa vijana 147 na kukabidhi vifaa vilivyotolewa na wadau mbalimbali ikiwemo Shirika la Maendeleo ya Ujerumani GIZ.

Amewataka vijana kutumia ujuzi walioupata kuzalisha bidhaa zenye ubora unaohitajika katika soko la kitaifa na kimataifa.

pharmacy

Msaki amesema kwa mwaka  2022/23 serikali imetenga Sh.Bilioni tisa, ili kuwezesha vijana kupata mafunzo ya ujuzi katika nyanja mbalimbali kwa lengo la kujikwamua kiuchumi.

“Jukumu la serikali ni kuhakikisha kunakuwepo sera na mipango ya kuwaongoza vijana ili wajiajiri, kuweka miundombinu sahihi ya kuwawezesha vijana kufanya shughuli za kiuchumi na kuhamasisha wadau kuhakikisha vijana wanafanya shughuli za kiuchumi,” amesema.

Naye, Meneja wa Mradi wa Jukwaa la Ushirikiano wa  Kimataifa (FIC), Erustus Ouko amesema lengo la mradi huo ni kushirikiana na serikali katika kusaidia kukuza ajira kwa vijana na wanawake.

Awali, Meneja wa Mradi wa Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ), Awadhi Milasi, amesema shirika hilo limechangia vifaa vyenye thamani ya Sh.Milioni 34 ili kufanikisha malengo ya Sido Dodoma hususani kuwainua wajasiriamali wadogo.

Meneja wa Sido   mkoa wa Dodoma, Twaha Sued alisema vijana 147 kati ya 151 waliosajiliwa wamehitimu mafunzo yao huku baadhi wakishindwa kuhitimu kwa sababu mbalimbali.

Mmoja wa wanufaika wa mafunzo hayo, Anthon Makasi amesema amepata  ujuzi ambao hakuwa nao awali na  kutoka kuwa mjasiriamali mdogo hadi kuwa  mkubwa na anatarajia kujiajiri baada ya mafunzo hayo.

Habari Zifananazo

Back to top button