SIMIYU: Mkuu wa Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu, Simon Simalenga amesema kuwa wafanyabiashara katika wilaya hiyo wameendelea kukaidi agizo la serikali la kufuata bei elekezi ya sukari na kuwauzia wananchi bei kubwa.
Simalenga amesema kuwa bei ya sukari ambayo wafanyabiashara wanawauzia wananchi kwa kilo moja ni kati ya Sh, 3,500 hadi 4,500 wakati bei elekezi katika wilaya hiyo inatakiwa kuwa kati ya Sh 2,800 hadi 3,000.
Mkuu huyo wa wilaya amesema hayo leo, wakati akizundua baraza jipya la biashara la wilaya, ambapo amewataka wafanyabiashara kuacha mara moja tabia hiyo na kufuata maelekezo ya serikali.
“ Serikali ilitoa bei elekezi ya Sukari nchi nzima na katika Wilaya yetu bei inatakiwa kwa kilo moja ni kati ya Sh, 28,000 hadi 3,000, lakini mpaka sasa wafanyabiashara mnawauzia wananchi kwa Sh. 3,500, hadi 4,500” amesema Simalenga
“ Jambo hili halikubaliki hata kidogo, hatutaweza kuwavumilia watu ambao wanaendelekea kukiuka maagizo ya serikali, niwatake wafanyabiashara wote, kufuata bei ekelezi ya sukari kama ambavyo imetolewa na serikali,” ameongeza Simalenga.
Mbali na hilo mkuu huyo wa wilaya amesema kuwa serikali itaendelea kutatua changamoto zote zinazowakabili wafanyabiashara, ikiwemo kuwawekea mazingira wezeshi ya ufanyaji wa shughuli zao.