‘Simamieni miradi ikamilike kwa wakati’

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amewataka wakuu wa idara katika halmashauri zote nchini wasimamie kikamilifu miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali kwenye maeneo yao na wahakikishe inakamilika kwa wakati, ili itoe huduma kwa wananchi kama ilivyokusudiwa.

Ameyasema hayo leo Jumatano, Februari 15, 2023  wakati akizungumza na watumishi wa Mkoa wa Songwe akiwa kwenye majumuisho ya ziara ya kikazi mkoani Songwe ya kukagua miradi ya maendeleo na mafanikio ambayo Serikali ya awamu ya sita imeyapata katika kipindi cha miaka miwili.

Amesema, huduma za jamii ndizo zinazogusa maisha ya kila siku ya wananachi kama elimu, maji, nishati, afya na kilimo, hivyo halmashauri zetu lazima ziongeze nguvu katika maeneo hayo.

“Wakuu wa Idara tumieni muda mwingi kwenda kwenye maeneo ambayo miradi inatekelezwa badala ya kukaa ofisini tu,” amesema Majaliwa.

 

Pia Majaliwa ameupongeza uongozi wa Halmashauri ya Mji Tunduma kwa kujenga baadhi ya miradi kwa kutumia makusanyo ya ndani, ukiwemo ujenzi wa madarasa 10 katika shule ya msingi Haisoja kwa gharama ya shilingi milioni 800, amewataka viongozi wa halmashauri zingine nchini kuiga mfano huo.

Pia amewaagiza wakaguzi wa elimu nchini wapite kwenye shule zote wakakague vitabu vinavyotumika katika shule hizo kama vinaendana na maadili na tamaduni za Kitanzania.

Majaliwa amewataka  viongozi wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kuongeza wigo wa kufanya tafiti za maeneo ambayo maji yatapatikana sambamba na kuongeza ulinzi kwenye vyanzo vya maji, ili kuhakikisha changamoto ya upatikanaji wa maji inatatuliwa.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Waziri Kindamba amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kuridhia fedha kiasi cha zaidi ya sh bilioni 190 kupelekwa mkoani humo kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maedndeleo ikiwemo ya afya sh. bilioni 47, maji sh. bilioni 30. 7, elimu sh. bilioni 32.9, nishati sh. bilioni 53.4 na barabara sh. bilioni 27.5

Habari Zifananazo

Back to top button