Simba, Azam viwanja tofauti nyumbani leo

LIGI Kuu Tanzania Bara inaendelea leo kwa mechi tatu kupigwa Dar es Salaam na Singida.
Wekundu wa Msimbazi, Simba itakuwa uwanja wa KMC, Dar es Salaam kuikaribisha Namungo kutoka mkoani Lindi.
Simba ipo nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi ikiwa na pointi 16 baada ya michezo saba wakati Namungo ni ya 13 ikiwa na pointi sita baada ya michezo saba pia.
SOMA: Makocha Simba, Coastal wategana
Wachimba dhahabu wa Chunya mkoani Mbeya, Ken Gold itakuwa mgeni wa Azam kwenye uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Azam ni ya tano ikiwa na pointi 15 baada ya michezo nane wakati Ken Gold inashika nafasi ya 16 mwisho wa msimamo ikiwa na pointi nne baada ya mechi nane pia.
Katika kipute kingine leo vinara wa ligi Singida Black Stars itakuwa mwenyeji wa Fountain Gate kwenye uwanja wa CCM Liti mjini Singida.
Singida Black Stars inaongoza ligi ikiwa na pointi 19 baada ya michezo saba wakati Fountain Gate ni ya nne ikiwa na pointi 16 baada ya mechi nane.



