Simba Queens yatoa winga Caf

WINGA wa kushoto wa Simba Queens, Opah Clement ni mmoja wa wachezaji 11 wanaounda kikosi bora cha Michuano ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika kwa upande wa wanawake, imeelezwa.

Kwa mujibu wa taarifa ya Shirikisho la Soka Afrika (Caf), kikosi hicho kimetangazwa baada ya kukamilika kwa mafanikio mashindano ya pili ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika kwa wanawake nchini Morocco na wenyeji ASFAR kutwaa ubingwa huo.

Simba katika mashindano hayo ilimaliza katika nafasi ya nne baada ya kutolewa katika nusu fainali kwa kufungwa bao 1-0 na Mamelod Sundows na baadaye kufungwa tena 1-0 na Bayelsa Queens ya Nigeria katika mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu.

Katika kikosi hicho, Opah yuko katika nafasi ya winga wa kushoto, huku wachezaji wengine walioteuliwa na Kamati ya Ufundi ya Caf baada ya kufanya vizuri katika nafasi zao ni kipa Khadija Errmichi wa ASFAR, ambaye pia alichaguliwa kuwa kipa bora wa mashindano hayo.

Er-rmichi alicheza mechi tano bila kuruhusu bao lolote wakati akiisaidia timu yake kutwaa ubingwa huo. Kwa upande wa mabeki, Mamelodi Sundowns imetoa Bambanani Mbane wakati ASFAR imemtoa Aziza Rabbah.

Ghizlane Chhiri wa ASFAR ni beki wa kushoto, wakati Glory Edet wa Bayelsa Queens amekuwa beki wa kulia. Wakati huohuo, kikosi cha Simba Queens kimewasili salama usiku wa kuamkia jana kikitokea nchini Morocco kilipokuwa kwa ajili ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa wanawake iliyomalizika Novemba 13, 2022.

Timu hiyo ambayo imeshiriki michuano hiyo iliyoanza msimu uliopita kwa mara ya kwanza na kufanikiwa kutinga nusu fainali, imerejea na zawadi ya kitita cha Dola za Marekani 200,000 (zaidi ya Sh milioni 460) ya kucheza nusu fainali pamoja na Dola 100,000 zawadi ya mshindi wa nne.

Katika michuano hiyo, wenyeji AS FAR walitawazwa mabingwa wapya kwa kuitungua Mamelodi mabao 4-0 na kuzoa kitita cha Dola za Marekani 400,000 huku mshindi wa pili akijinyakulia Dola 250,000.

Habari Zifananazo

Back to top button