Singida yapokea bil 34.9/- kuimarisha sekta ya afya

MKOA wa Singida umepokea Sh 34,988,762,952.2 za kuimarisha sekta ya afya katika kipindi cha miaka miwili ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita.

Mkuu wa Mkoa, Peter Serukamba amesema kati ya fedha hizo Sh bilioni 8.9 na vyanzo vingine zilitokana na tozo za miamala ya simu kwa ajili ya ujenzi wa vituo 20 vya afya. Baadhi ya vituo hivyo vilitajwa na Serukamba kuwa ni Ntuntu, Chibumagwa, Ilunda, Gumanga, Mandewa, Urugu, Kisiriri, Mwanduijembe, Iyumbu, Unyambwa, Sanza, Makuro, Makulu na Mtipa.

“Shilingi 6,650,000,000 zilipokewa kwa ajili ya kujenga hospitali mpya nne za Wilaya Ikungi, Mkalama, Singida na Itigi pamoja na kukarabati hospitali ya Wilaya ya Manyoni,” alisema Serukamba.

Alisema Sh 2,550,000,000 zilipokewa ili kukamilisha zahanati 51 zilizojengwa na wananchi, Sh 1,400,000,000 zilipokewa kwa ajili ya ujenzi wa majengo matatu ya dharura katika hospitali za wilaya za Iramba, Manyoni, Mkalama na majengo mawili ya wagonjwa mahututi yamejengwa katika hospitali za wilaya za Singida na Iramba.

Serukamba alisema makazi ya watumishi wa afya yameboreshwa na nyumba sita zimejengwa katika halmashauri za Itigi, Manyoni, Iramba, Mkalama na Singida kwa Sh 540,000,000.

Alisema walipokea Sh 2,050,000,000 za ununuzi wa vifaa tiba kwenye hospitali za wilaya, vituo vya afya na zahanati katika halmashauri za Iramba, Mkalama, Ikungi na Manyoni ili zianze kutoa huduma.

Ujenzi wa miundombinu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ulipokea Sh 11,833,184,333.30 na ilielezwa na Serukamba kuwa jengo la wagonjwa mahututi, jengo la dharura, nyumba ya mtumishi vimejengwa.

Pia alisema umefanyika ujenzi wa jengo tengefu la sakafu nne, umefanyika ununuzi wa vifaa tiba na ukarabati wa vyumba vya CT-Scan na Digital X-Ray pamoja na watumishi mafunzo maalumu kazini.

Alisema Sh 1,065,391,118.89 zilipokewa kwa ajili ya uhamasishaji wa chanjo dhidi ya ugonjwa wa Covid-19 ambapo wananchi 906,420 sawa na asilimia 102 walipatiwa chanjo hiyo.

 

Habari Zifananazo

Back to top button