PEMBA : RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dk. Hussein Ali Mwinyi, amezindua meli ya kwanza ya makontena katika Bandari ya Mkoani na kuwataka wafanyabiashara kutumia fursa hiyo kuifungua Pemba kiuchumi.
Rais Dk. Mwinyi ameshuhudia meli ya Lamu Shipping Limited ikishusha kwa mara ya kwanza makontena kwenye Bandari ya Mkoani, hatua aliyoielezea kuwa ni mapinduzi makubwa kwa sekta ya usafirishaji hapa nchini.
Akizungumza na wananchi katika eneo la Bandari Kavu ya Mkoani, Mkoa wa Kusini Pemba., Dk. Mwinyi ameeleza kuwa kinachofanywa na Serikali si kuzikodisha bandari kwa kuendelea kushirikiana na sekta binafsi ili kuongeza tija na ufanisi katika uendeshaji wa majukumu ya bandari zote nchini.
Aidha, amefahamisha kuwa hatua ya kuanza kushushwa kwa makontena kwenye bandari hiyo itarahisisha na kupunguza gharama za usafirishaji na kuwaondolea wafanyabiashara mzigo wa gharama kubwa.
Rais Dk. Mwinyi amewahakikishia wananchi wa Pemba kuwa Serikali inaendelea na mipango ya kukamilisha ujenzi wa uwanja wa ndege wa Pemba utakaoanza hivi karibuni, pamoja na ujenzi wa bandari za Shumba, Wete, na Bandari ya Mangapwani, Unguja, ambayo ameielezea kuwa itakuwa na uwezo wa kuhudumia meli nyingi zaidi katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Rais Dk. Mwinyi ameeleza kuwa hatua hiyo ya kuifungua Bandari ya Mkoani itaambatana na ujenzi wa maghala ya kuhifadhia bidhaa za wafanyabiashara, viwanda vidogo vya kuchakata mwani na mazao ya baharini, pamoja na majokofu. Amehimiza wananchi wa Pemba kuchangamkia fursa hizo.
SOMA: Dkt Mwinyi akutana ujumbe Oman Zanzibar
Wakati huo huo, Rais Dk. Mwinyi ameshuhudia makabidhiano ya Bandari ya Mkoani baina ya Shirika la Bandari na Kampuni ya Fumba Port Limited kwa ajili ya kuimarisha uendeshaji wake.