SMZ kulinda urithi wa hifadhi Mji Mkongwe

Eneo la Mji Mkongwe, Zanzibar

RAIS wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema serikali yake inaendelea kulinda urithi wa hifadhi ya kimataifa ya Mji Mkongwe kwa kuzingatia kanuni na taratibu zilizowekwa.

Dk Mwinyi alisema hayo Ikulu, Zanzibar jana alipokutana na ujumbe kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kujadili kuhusu utunzwaji wa hifadhi ya kimataifa ya Mji Mkongwe.

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imechukua hatua kutunza urithi wa Mji Mkongwe ikiwa ni pamoja na kuondoa maegesho ya vyombo vya moto kwenye maeneo yote ya Mji Mkongwe ili kuenzi na kuufanya uendelee kuwa kivutio mashuhuri cha watalii.

Advertisement

Dk Mwinyi alisema katika kutekeleza hatua hiyo, serikali imeamua kujenga maegesho ya vyombo vya moto eneo la darajani ikiwa ni njia mbadala ya kuondosha msongamano katika eneo la Mji Mkongwe.

Pia alieleza mikakati ya serikali kushirikisha sekta binafsi katika kulinda urithi huo kwa kukarabati majengo chakavu kwa mujibu wa kanuni na taratibu bila kuharibu urithi wake na kuyarudisha katika uhalisia wake.

Alisema SMZ kwa kushirikiana na Serikali ya Oman wanaendelea na kusimamia ujenzi wa majengo ya Beit Al Ajaib na People’s Palace ambayo ni alama inayoitambulisha Zanzibar duniani kote.

1 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *