SMZ kuongeza bajeti ya elimu Tril 1

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imepanga kuongeza bajeti ya sekta ya elimu kutoka shilingi bilioni 864 hadi kufikia shilingi trilioni 1, ili kuimarisha ubora wa elimu na kupanua miundombinu ya sekta hiyo nchini.
Akizungumza leo, Desemba 5, 2025, kwenye ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa 13 wa Jumuiya ya Walimu Wakuu wa Skuli za Sekondari za Zanzibar (JUWASEZA) uliofanyika katika ukumbi wa Skuli ya Fidel Castro, sambamba na uzinduzi wa Dakhalia mpya ya wanafunzi wa kike Mkoa wa Kusini Pemba, Dk. Mwinyi alisema Serikali inatekeleza mikakati ya kuboresha mazingira ya ufundishaji, maslahi ya walimu na ujenzi wa miundombinu ya kielimu.

Amesema ujenzi wa Dakhalia hiyo ni sehemu ya mpango wa Serikali wa kuimarisha elimu, akibainisha kuwa lengo ni kujenga Dakhalia katika kila wilaya ili kufikia wanafunzi 10,000 watakaosoma katika skuli za Dakhalia ifikapo mwaka 2030. Rais Mwinyi aliwataka walimu wakuu kusimamia kwa weledi miundombinu, ufaulu na matumizi sahihi ya rasilimali za umma, huku akiahidi kutenga fedha za ukarabati pale itakapohitajika.
Kwa upande wake, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Lela Mohamed Mussa, alisema mageuzi yanayoshuhudiwa katika sekta ya elimu yanatokana na maono ya Rais Mwinyi katika kusukuma mbele maendeleo ya elimu Zanzibar.

Naye Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Khamis Abdallah Said, amesema ujenzi wa Dakhalia ya Skuli ya Fidel Castro umegharimu shilingi bilioni 1.5 na ina uwezo wa kuchukua wanafunzi 288, huku wizara ikipanga kujenga Dakhalia nyingine 16 Unguja na Pemba katika mwaka wa fedha 2025/2026.
Mradi huo wa Dakhalia ya wanafunzi wa kike wa Skuli ya Fidel Castro ni wa kwanza kufunguliwa na Dk. Mwinyi kisiwani Pemba tangu aingie katika kipindi chake cha pili cha uongozi wa Awamu ya Nane. SOMA: Bilioni 518 kuendeleza elimu Zanzibar



