SMZ yajivunia kuacha alama utekelezaji wa ilani

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imesema imeweka alama kwa Wazanzibari katika utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
SMZ imesema utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM umegusa kila mwananchi katika shehia zote 388, wilaya zote 22 na mikoa 11 ya serikali na kichama.
Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla alisema hayo kwenye Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM Dodoma jana wakati akiwasilisha utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020/2025 kwa upande wa Zanzibar.
Abdulla alisema serikali ya CCM katika miaka mitano ilionesha dhamira ya kujielekeza katika misingi ya kuinua Wazanzibari kiuchumi, kisiasa na kijamii.
Alisema uchumi wa SMZ ndani ya miaka mitano imekua kutoka katika asilimia 1.3 mwaka 2020 hadi asilimia 7.4 mwaka 2024
Abdulla alisema pato la taifa limeongezeka kutoka Sh trilioni 4.78 kwa mwaka 2021 hadi Sh trilioni 6.573 mwaka 2024 na kuna ongezeko la asilimia 145.7 katika ukusanyaji wa mapato ya ndani.
SMZ ilisema katika sekta ya afya imeendelea kuimarisha huduma za afya kwa kukamilisha hospitali 10 za wilaya na moja ya mkoa zenye vifaatiba vya kisasa Unguja na Pemba kwa bajeti ya Sh bilioni 104.44.
Alitaja hospitali hizo ni Kipunge, Panga Tupu, Kitogani,Mwera Pongwe, Jitimai, Mbozini na Chunguni kwa Unguja na kwa Pemba ni Vitongoji, Michaweni na Kinyasini.
Abdulla alisema bajeti ya sekta ya afya iliongezeka kutoka Sh bilioni 265.5 mwaka 2021/22 hadi Sh bilioni 830 mwaka 2024/25 sawa na ongezeko la asilimia 212.6.
Alisema elimu imeboreshwa kwa ujenzi wa shule 149 za maandalizi za msingi na sekondari zenye madarasa 4,810 na kwamba shule 60 ni za ghorofa.
Abdulla alisema serikali imetimiza dhamira ya kumtua mama ndoo kichwani kwa kuimarisha huduma za maji kwa ujenzi wa tangi na ulazaji wa mabomba na kufanya wananchi kupata uhakika wa maji safi na salama kwa asilimia 88.2.
Alisema serikali imesambaza umeme katika vijiji 231 vikiwemo 144 vya Unguja na 37 vya Pemba sawa na asilimia 76 ya vijiji 305 vilivyotakiwa kuunganishwa na huduma hiyo.
Abdullah alisema katika miundombinu SMZ imejenga upya barabara zilizochoka, imejenga madaraja yakiwemo ya juu, imeboresha kiwanja cha ndege, imeimarisha bandari katika maeneo mbalimbali.
Pia alisema SMZ imejenga masoko, vituo vya daladala, imewekeza Sh bilioni 29 katika uchumi wa buluu na Sh bilioni tano katika uwezeshaji wa wananchi kiuchumi.