SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imesema sera ya pamoja ya Tanzania bara na Zanzibar ni muhimu katika kuzitumia fursa za uchumi wa buluu.
Katibu Mkuu Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar, Dk Aboud Jumbe alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN), katika Ofisi za Makao Makuu ya Kampuni hiyo Tazara Dar es Salaam.
Dk Jumbe alisema katika sera hiyo changamoto ni kubwa zaidi Tanzania bara kwa kuwa lazima iwepo programu inayoangalia uchumi wa buluu katika ukanda wa bahari kutoka Tanga – Mtwara hadi Ruvuma sanjari kuangalia uchumi wa buluu katika Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika na Ziwa Nyasa.
“Hizi ndizo shared interest ambazo kwa pamoja zikiwemo ndani ya sera hii ya Jamhuri ya Muungano sio tu kwamba itazidi kuisaidia Zanzibar katika programu yake ya uchumi wa buluu lakini pia Jamhuri ya Muungano kwa pamoja”alisema.
Aliongeza“Cha muhimu ni kwamba hivi sasa Jamhuri ya Muungano ipo njiani inatengeneza sera ya uchumi wa buluu hii itakuwa ni sera yetu moja mpaka Zanzibar kwa sababu tayari tumeshatuma wadau wetu kutoka SMZ na Bara tumekutana Arusha tumefanya kazi kubwa ya kujenga hii sera ambayo itaipaisha zaidi Jamhuri ya Muungano na kuiweka mbele zaidi katika safu za usimamizi wa masuala ya bahari na uchumi wa buluu,”
Dk Jumbe alisema Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu Tanzania ni moja kati ya vitovu vikuu vya uchumi wa buluu na usimamizi wa bahari katika uvuvi wa bahari kuu na usalama wa bahari huyo.
Alisema ushirikiano wa pamoja unaleta tija katika faida katika kufanya kazi kwa pamoja na msimamo wa pamoja katika masuala ya uvuvi wa kikanda au maazimio ya uvuvi wa ulimwengu
“Kwa uchumi wa buluu ni muhimu sana kwa Jamhuri kuwa kitu kimoja katika suala zima la msimamo katika Kanda, katika safu za kimataifa lakini pia utekelezaji wa Ilani ya chama kote kote Bara na Zanzibar katika kuendesha program zake za uchumi wa buluu,” alisema.