SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), imesema kuwa Ukanda wa Magharibi wa Bahari ya Hindi una fursa ya kuvuna kiasi cha dola bilioni 300 (sawa na Sh trilioni 699.14) zinazotokana na uchumi wa buluu.
Katibu Mkuu Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Zanzibar, Dk Aboud Jumbe alisema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN), katika Ofisi za Makao Makuu ya Kampuni hiyo Tazara Dar es Salaam.
Dk Jumbe alizitaja nchi 10 zilizopo katika ukanda huo ni Somalia, Kenya, Tanzania, Msumbiji, Afrika Kusini, Madagasca, Comoro, Mauritius, Seychelles na Ufaransa.
Alisema kiasi hicho cha dola bilioni 300 ni kwa mujibu ya tathmini iliyofanywa miaka mitano iliyopita kuwa katika nchi hizo 10 kuna fursa hiyo, japo kinachotumika ni fursa ya bilioni 20 tu.
Dk Jumbe alisema fursa hizo zinazotoa dola bilioni 20 zinatokana na shughuli za utalii kwa kuwa shughuli za usafiri wa bahari bado nchi hizo hazijaweza kuweka ajenda ya pamoja.
“Dola bilioni 20 kwa mwaka ni kidogo kutokana na assessment (makadirio) iliyofanyika. Bado nchi hizi hazijaweza kufikia huko ndio maana tunakaa kwa pamoja, tunakutana, tunaunda sera ya mkakati wa kikanda ya usimamizi wa bahari ambayo itachukua maeneo yote ikiwemo uchumi wa buluu, uvuvi, usafiri wa baharini, utalii na hifadhi ya bahari,” alisema.
Dk Jumbe alisema SMZ imetoa shilingi bilioni 36 kuwezesha wavuvi wadogo, wakulima wa mwani, wafugaji wa kaa, wafugaji wa majongoo bahari na wakoshaji wa dagaa ikiwa ni sehemu ya mikakati ya uchumi wa buluu.
Alisema uwezeshaji huo ni sehemu ya fedha ilizopata SMZ kutoka kwenye mkopo uliotolewa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kukabili athari za janga la Covid-19.
Alisema kila nchi katika uchumi wa buluu una malengo yake, lakini Zanzibar imeona iwawezeshe wananchi wake waweze kufanya shughuli zao kwa urahisi katika kuwasaidia kuwapa uelewa, mbinu, zana., mitaji na masoko katika maeneo yao ya uvuvi mdogo mdogo.
“Tanzania dhana yake ni kumwezesha mtanzania ambaye kila siku anahangaika na maisha sisi hatuwezi kuifikia dhana ya uchumi wa buluu ikaingia majumbani mwa watu ikiwa mwananchi mwenyewe hajaelewa faida ya dhana hiyo lakini pia haoni jitihada za serikali ya kumsaidia” alisema Dk Jumbe.