UTEKELEZAJI wa mradi wa Soko Kuu la Jiji la Mwanza umefikia asilimia 96 na ni kivutio kwa wakazi wa jijini Mwanza hasa wafanyabiashara.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Sekiete Yahaya amesema ujenzi wa soko hilo ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya 2020- 25 na Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa miaka mitano (2021/22- 2025/26).
Yahaya alilieleza HabariLEO kuwa miongozo hiyo inasisitiza ujenzi wa uchumi shindani wa viwanda.
Ilani ya CCM katika ibara yake ya 24 (a) inasisitizwa kutengwa kwa maeneo kwa ajili ya wajasiriamali wakiwamo mama lishe, wauza mboga na wanyabiashara wadogo ili kuyawezesha makundi hayo kufanya shughuli zao bila bugudha.
Yahaya alisema kwa mujibu wa mkataba, mradi huo ulianza kutekelezwa Oktoba, 2020 na ulitarajiwa kukamilika Aprili mwaka huu, lakini kutokana na changamoto mbalimbali zilizojitokeza haukuweza kukamilika kwa wakati.
Alitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na kuwapo kwa chemchemi kwenye eneo la mradi iliyosababisha mchoro wa msingi wa mradi huo kubadilishwa ili uendane na hali ya eneo.
Yahaya alitaja changamoto nyingine kuwa ni vifaa vya ujenzi kutopatikana kwa wakati hali iliyosababishwa na ugonjwa wa Covid-19 hivyo mkandarasi kuomba kuongezewa muda wa kukamilisha mradi hadi Septemba 18 mwaka huu.
“Maombi ya kuongezewa muda yaliwasilishwa mwezi Machi 2022 na yapo katika hatua mbalimbali za maamuzi,” alisema.
Yahaya alitaja kazi za ujenzi zilizofanyika hadi sasa kuwa ni ujenzi wa jengo la soko, msingi wa jengo ghorofa ya chini upande wa chini ambao umekamilika kwa asilimia 100 na ghorofa ya chini upande wa kulia iliyokamilika kwa asilimia 87.
Alitaja kazi nyingine zilizofanyika na asilimia kwenye mabano ni pamoja na ujenzi wa handaki (50), ghorofa ya kwanza (100), maduka ya kuzunguka pande mbili za soko (60), umwagaji wa nguzo za kwenda kubeba kenchi za paa (100), vizimba (90), uwekaji wa kechi (40) na ujenzi wa maduka ghorofa ya kwanza asilimia 20.
Alisema gharama ya ujenzi wa soko hilo la kisasa lililo katika Kata ya Pamba ni Sh 20,739,695,080 na hadi sasa jumla ya Sh 13,131,504,940.58 zimetumika ikiwa ni sawa na asilimia 78. Mhandisi Mshauri akiwa amelipwa Sh 1,383,200,186.80 kati ya Sh 1,721,994,671.55, fedha ambazo zilisainiwa kwenye mkataba wa ujenzi wa soko hilo.
Yahaya alisema mradi huo unatarajia kuwa na eneo la maegesho ya magari madogo 192 chini ya ardhi, maduka 400 yakiwamo madogo, ya kati na makubwa ndani ya jengo hilo la soko.
Alisema mradi huo wa soko utasaidia kuongeza mapato ya halmashauri, utalifanya Jiji la Mwanza kuwa la kisasa zaidi na utasaidia kukua kwa biashara nyingine kutoka kwa wafanyabiashara wa ndani, mikoa na nchi jirani.
“Mradi huu umetoa ajira kwa vijana wapatao 175 ambao wanaendelea na kazi mbalimbali za ujenzi,” alisema Yahaya.
Alitaja changamoto zilizojitokeza kuwa ni upatikanaji mgumu wa baadhi ya vifaa vilivyokuwa vinaagizwa kutoka nje ya nchi kuchelewa kufika kwa wakati bandarini na hivyo kuathiri kasi ya utekelezaji wa mradi. “Upandaji holela wa bei za vifaa vya ujenzi nayo ilikuwa changamoto katika utekelezaji wa mradi huu,” alisema Yahaya.
Mwenyekiti wa Soko Kuu la Mwanza, Hamadi Nchola aliishukuru serikali kwa kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa soko hilo ambalo linakwenda kukuza uchumi kwa wakazi wa Jiji la Mwanza.