Sokoine ameacha alama kukemea rushwa

PAROKO wa Kanisa Katoliki Parokia ya Emairete Kigango cha Engwikie Monduli Juu Wilayani Monduli , Arnold Baijukie amesema kuwa hayati Edward Sokoine ni kiongozi aliyeacha alama na kukemea masuala ya rushwa ikiwemo uhujumu uchumi.
Akiongoza ibada ya kumbukizi ya miaka 39 ya kifo cha Sokoine, Paroko Baijukie, alisema lengo la kuadhimisha kumbukumbu ya kifo cha marehemu Sokoine kilichotokea Aprili 12,1984 ni alama aliyoiacha katika historia ya nchi ya Tanzania.
“Tunamkumbuka Sokoine kwa sababu aliacha alama aliyoweka katika familia yake na Taifa kwa ujumla sababu alisimamia haki ikiwemo kupambana na wahujumu uchumi,” amesema na kuongeza:
“Tunaomba ndoto alizotuachia tuzimalize kwa kujenga shule kwa ajili ya kuinua elimu kwa jamii za kifugaji, natoa rai kwa wake wa marehemu kutokuwa wanyonge.”
Baada ya misa ya shukrani ya maisha ya kukumbuku ya marehemu, salam mbalimbali zilitolewa, ambapo Askofu wa Kanisa la Kilutheri Afrika Mashariki (KKAM), Philemon Lengasi amemuomba Rais Samia Hassan Suluhu kuchukua hatua kwa wale wote waliotajwa katika ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali, kwani pia hayati Sokoine alipinga masuala ya rushwa na uhujumu uchumi.
Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Joshua Nassari, amesisitiza suala la elimu kwa jamii ya wafugaji na kueleza mkuwa watoto hawawezi kutumikishwa kulisha mifugo, lazima wasome, ili kujikwamua kiuchumi.
Na Shekhe wa Wilaya ya Monduli, Ahmed Kisanda ameomba serikali iboreshe zaidi maktaba zote nchini ili watu mbalimbali wasome vitabu na kumbukumbu ya viongozi mbalimbali waliofanya mambo mengi katika nchi hii.