Suala la muda tu Lameck lawi kutua Simba, Azam FC

TANGA: KLABU ya Coastal Union imethibitisha kupokea ofa kutoka timu tatu za Ligi Kuu Tanzania bara wakiwemo Simba SC, Azam FC na Ihefu FC zote zikihitaji huduma ya beki Lameck Lawi ambaye amekuwa na kiwango kizuri ndani ya kikosi cha Wagosi wa Kaya kwa msimu huu wa 2023/2024.

Akizungumza na waandishi wa habari Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Coastal, Abdallah Unenge amesema wamezipokea ofa hizo na alibainisha kuwa kuna ofa ambazo zimekwisha jibiwa huku wakiendelea kujadili na ikitokea itakayokidhi vigezo basi Wanamangushi hao wapo tayari kumuuza.

” Ni kweli Lameck Lawi anafuatiliwa na mpaka sasa vilabu vya Simba , Ihefu na Azam zimeleta ofa rasmi mezani na zinaendelea kujadiliwa baadhi yao tumeshawajibu kulingana na matakwa yetu wakifika kwenye kile ambacho tunakihitaji basi biashara itafanyika” amethibitisha Unenge.

Advertisement

Amesema kuwa uwepo wa Lameck Lawi katika safu ya ulinzi ndani ya Coastal Union umekuwa na tija kwa klabu lakini ni lazima ifike mahali kumpa Uhuru mchezaji kama atahitaji kutafuta changamoto sehemu nyingine.

“Haja ya kumbakisha Lameck Lawi katika kikosi chetu tulikuwa nayo lakini mpira ni maisha sisi tumebakia na mwaka mmoja naye yawezekana ofa ambayo vilabu vingine vimepanga imemshawishi mchezaji sasa wakati mwingine kwenye mpira lazima uangalie ni wapi unapata faida” amesema Unenge.