SUA wampongeza Samia kudumisha amani

MOROGORO; CHUO Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), kimempongeza Rais  Samia Suluhu Hassan kwa kudumisha amani, upendo na mshikamano kwa Watanzania.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu hicho , Profesa  Raphael Chibunda ametoa pongezi hizo wakati wa futari iliyoandaliwa na SUA  kwa wanajumuiya wa dini ya Kiislam wanaofanya kazi chuoni hapo na viongozi mbalimbali wa dini hiyo mkoani Morogoro.

Amesema umoja, mshikamo na amani iliyopo nchini haitokei hivi hivi, ila ni jitihada za makusudi zinazofanywa na serikali na ndiyo maana unaweza kuona pamoja na kuwa futari imeandaliwa kwa wanajumiya wa chuo, lakini maandalizi yake yameshirikisha watu wa imani zote.

Advertisement

“Nitumie fursa hii kumpongeza Rais wetu  Dk  Samia Suluhu Hassan kwa kudumisha amani, upendo na mshikamano unaotuweka pamoja katika ushiriki wa mambo mbalimbali,” amesema Profesa  Chibunda.

Amesema chuo hicho  kimekuwa na utaratibu wa kuandaa futari kwa waumini wa dini ya Kislam kila mwaka wakati wa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Akitoa salamu za Baraza Kuu la Waislam Tanzania (BAKWATA) Mkoa wa Morogoro, mwakilishi wa Sheikh wa Mkoa,  ambaye pia ni Sheikh wa Wilaya ya Morogoro, Sheikh  Jafari Thenei amesema SUA ni chuo cha kuigwa, kwani kimekuwa na utaratibu mzuri wa kuwakutanisha Waislam na huo ni upendo.

Amesema tendo la kuwafuturisha wanajumuiya ya Kiislam chuoni na waumini wa dini hiyo, ikiwemo viongozi wa mkoa na wilaya linalofanywa kila mwaka linaendelea kujenga upendo na mshikamo kati ya chuo hicho na waumini wa dini hiyo wa ndani na wa nje.