UJERUMANI : WAZIRI wa Maendeleo ya Uchumi wa Ujerumani, Svenja Schulze amezungumzia janga kubwa la kibinadamu nchini Sudan kufuatia ziara yake ya hivi karibuni katika eneo hilo, na kuisifu Chad kwa mshikamano licha ya umaskini.
Katika mahojiano maalumu na DW Afrika, Schulze alielezea hali ilivyo kwenye mpaka wa Sudan na Chad, ambako maelfu ya wakimbizi, hasa wanawake na watoto, wamekimbia machafuko.
Ameisifu Chad kwa mshikamano wake licha ya kuwa moja ya nchi masikini zaidi, na kuiomba dunia kuanza kuchukua hatua. SOMA: Wanawake Sudan njiapanda udhalilishaji kingono
Schulze pia amebainisha kuwa mgogoro huo umepuuzwa kutokana na migogoro ya Mashariki ya Kati na Ukraine, akitoa wito kwa uhamasishaji mkubwa wa kimataifa na shinikizo kwa pande husika.
Amesema Ujerumani itaendelea na msimamo wake wa kuzuia silaha kufika kwenye mgogoro huo na kusisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa, hasa na Umoja wa Afrika, kukabiliana na mgogoro huo wakati Marekani inapojiondoa kwenye dhima hiyo.