Taa ya Lincoln iliyozimwa kwa risasi

LEO katika historia tunarudi miaka 158 nyuma hadi mwaka 1865 kuangazia tukio la simanzi kwa mpenda demokrasia, mwanaharakati wa haki na usawa wa watu wote ulimwenguni aliyetambulika kama baba wa demokrasia. 

Huyu ni Rais wa 16 wa Marekani Abraham Lincoln. Lincoln alizaliwa Februari 12, 1809 mji wa Hodgenville Jimbo la Kentucky mwanaume mrefu wa futi 6.4

Alikuwa ni mwanasheria, kiongozi wa Chama cha Whig, Mbunge wa Illinois, pia mjumbe wa Congress pia ni mwanamieleka hodari aliyepigwa mara moja tu maishani katika mapambano yanayokadiriwa kufika 300.

Alifahamika kwa Jina la umaarufu ‘Honest Abe’ kutokana na sifa yake ya kuwa mkweli na muaminifu katika kofia zote mbili, siasa na sheria.

Alipendelea kuvaa kofia ndefu kichwani iliyobatizwa ‘Top Hats’, ambayo mara kadhaa aliitumia kuhifadhia nakala mbalimbali ndani mwake kofia ambayo imetunzwa hadi leo katika Makumbusho ya kihistoria huko Washington DC.

Atakumbukwa kama kiongozi aliyepinga na kusababisha kukoma kwa biashara ya utumwa ulimwenguni

Hii ni baada ya vuguvugu la vita vya kiraia ‘American Civil Rights 1865’, alitoa hotuba aliyoibatiza Jina la ‘Emancipation proclamation ‘, yaani tangazo la ukombozi, ambapo katika moja ya nukuu ya hotuba hiyo nanukuu: “That all persons held as slaves, within the rebellious states are, and henceforward shall be free.”

Kwa tafsiri isiyo rasmi: Watu wote wanaoshikiliwa kama watumwa ndani ya nchi zilizoasi kuanzia sasa wapo na watakuwa huru.”

Kama alama ya heshima Lincoln ni mmoja kati ya marais wa nne pekee taswira zao kuchongwa katika mlima Rushmore, sambamba na baba wa taifa hilo hayati Rais George Washington, Thomas Jefferson na Theodore Roosevelt.

Katika moja ya hekalu kubwa la kale pale Washington DC kuna sanamu la Lincol katikati yake likichagizwa na ujumbe maridhawa; “In this temple as in the in the hearts of the people for whom he saved the union, the memory of Abraham Lincoln is enshrined forever. “ 

“Katika hekalu hili, kama ndani ya mioyo ya watu ambao aliokoa muungano, kumbukumbu ya Abraham Lincoln imehifadhiwa milele.” 

Alichotumwa duniani kilitamatika mwaka wa nne wa urais wake 1865.

Kwani alifariki kwa kupigwa risasi kisogoni na muigizaji John Wilkes katikati ya uhondo wa maigizo ya vichekesho katika ukumbi wa sinema wa Ford.

Popote usomapo mafunzo ya demokrasia katika taasisi, shirika ama chuo chochote duniani lazima utapitia nukuu yake isemayo; “Democracy is a government of the people, by the people, and for the people.”

Habari Zifananazo

Back to top button