WATOTO 120 wanaoishi katika mazingira magumu mkoani Kigoma wanatarajia kupata unafuu wa maisha, baada ya Shirika la Maendeleo ya Vijana Kigoma (KIVIDEA) kuanza kutekeleza mpango wa kugharamia elimu ya watoto hao.
Mkurugenzi Mtendaji wa KIVIDEA,Babu Pascal akizungumza katika maadhimisho ya siku ya familia duniani yaliyofanyika katika manispaa ya Kigoma Ujiji alisema kuwa shirika hilo linatarajia kutumia kiasi cha shilingi milioni 586 katika kutekeleza mpango huo wa elimu kwa watoto hao.
Pascal alisema kuwa utekelezaji wa mpango huo unafuatia ufadhili uliotolewa na shirika la la terre des hommes schweiz (tdhs), ambapo Mkurugenzi huyo alisema kuwa kwenye idadi hiyo ya watoto watakaonufaika imegawanywa nusu kwa wanafunzi wasichana na nusu wanafunzi wavulana.
Alisema kuwa mradi huo utafanya kazi katika Kata za Uvinza, Ilagala, Kazuramimba na Nguruka zilizopo halmashauri ya wilaya Uvinza na kata tisa za Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji.
Sambamba na mahitaji ya elimu, mradi huo pia utahusisha watoto kukatiwa bima ya afya, kuhamasisha na kuwashauri wazazi na walezi kuchangia mahitaji mengine muhimu ikiwemo chakula na malazi.
“Tayari matunda ya utekelezaji wa mradi yameanza kuonekana ambapo wapo watoto 23 wamefaulu mitihani ya darasa la saba na kuchaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza huku wanafunzi wengine watatu wakifaulu mitihani ya kidato cha nne na kuchaguliwa kuendelea na masomo ya kidato cha tano na sita,” alisema Babu Pascal.
Akizungumza katika maadhimisho hayo Mkuu wa Mkoa Kigoma,Thobias Andengenye alisema kuwa malezi duni ya wazazi na mimba kwa wanafunzi vimefanya wanafunzi wengi kupoteza ndoto zao za kupata elimu bora na maisha bora hivyo wengi wamekimbia nyumbani na kuishi mitaani.
Katika hotuba iliyotolewa kwa niaba yake na Mkuu wa Wilaya Kigoma, Salum Kalli alisema kuwa kwa kigezo cha umasikini na kuondoka nyumbani na kuacha familia kwa kigezo cha kwenda kuhangaika kutafuta maisha wazazi, wamewaacha watoto wao na watoto kujilea wenyewe wakifanya kila jambo ambalo wanaliona kwao sawa hata kama ni kinyume cha maadili.
Comments are closed.