Taasisi ya Celina Kombani yasaidia wanafunzi Moro

MOROGORO; WANAFUNZI 1,200 wa darasa la kwanza shule za msingi kwenye halmashauri tisa za mkoa wa Morogoro wanatarajia kunufaika kupatiwa madaftari na penseli kupitia Taasisi ya Celina Kombani Memorial Foundation, ukiwa ni mkakati wa kuunga mkono juhudi za serikali uboreshaji wa elimu nchini .
Kwa kuanzia utekelezaji huo, wanafunzi 300 wa shule za msingi sita kutoka halmashauri mbili ya Manispaa ya Morogoro na Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro kila mmoja amepatiwa daftari sita, penseli na ufutio.
Mhasibu wa taasisi hiyo, Joyce Mizambwa kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji, Lucy Kombani ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Morogoro, amesema taasisi imekijita kusaidia wanafunzi kielimu.
Amesema inawasadia kuwapa elimu na ujuzi ambao wanautumia kama ajira ya kuwawezesha kupata kipato, ili kuisaidia serikali kupambana na changamoto za ajira.

Amesema mwaka huu taasisi imeanza ugawaji wa madaftari katika shule za msingi na awamu ya kwanza imehusishwa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro na Manispaa ya Morogoro.
Katika Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro wanafunzi wa darasa la kwanza waliowezeshwa ni Kikundi Kijijini, Lukonde na Juhudi ,wakati Manispaa ya Morogoro ni Towelo, Kaloleni na Tungi.

Naye Mjumbe wa Bodi ya taasisi hiyo, Dorisia Edward ametoa wito kwa wazazi na walezi kushiriki kikamilifu kwenye kuchangia chakula shuleni, ili wanafunzi hasa wa darasa ka kwanza waweze kupata mlo na kuwafanya wawe na ufanisi mzuri katika masomo



