Taasisi yatoa misaada kwa wenye ulemavu

TAASISI ya Mama Ongea na Mwanao imetoa zaidi ya baiskeli za viti mwendo 50, pikipiki mbili, zawadi na vyakula kwa watu wenye ulemavu kupitia kampeni ya “Asante Mama umetufikia” kulitia moyo kundi hilo linalokutana na changamoto mbalimbali za kimaisha.
Taasisi hiyo iliyoko chini ya wasanii imefanya tukio hilo jijini Dar es Salaam huu ukiwa ni mwaka wa tatu wakiunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan za kuyatambua makundi yote na kuyasaidia.
Akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi baiskeli hizo Mwenyekiti wa Taasisi ya Mama Ongea na Mwanao Steven Mengele ‘Steve Nyerere’ amesema kundi hilo na hasa wanawake wamekuwa wakiachiwa majukumu ya kulea watoto wenye ulemavu na wengine wanatelekezwa.
“Rais Samia kwa kuona namna baadhi ya watu wanapata shida kwa kuachiwa majukumu ya kulea wenye ulemavu akasema kaeni nao, kuleni nao, kunyweni nao na kuhakikisha wanapata furaha, Rais ni mama anajua mapito ya mtoto wake na kulea familia bora,”alisema.
Steve Nyerere alihimiza jamii kutowafungia watoto wenye ulemavu ndani kwani nao wana haki ya kupata elimu hivyo wawatoe nje.

Pia, aliwashukuru wadau mbalimbali waliomuunga mkono katika kuchangia mahitaji ya wenye ulemavu kupitia taasisi hiyo akisema wapo waliotoa fedha, jezi, mpira, vyakuka na baiskeli na kuahidi mwaka huu mpya wataenda katika mikoa mbalimbali kuwasaidia wenye ulemavu.
Meya wa jiji la Dar es Salaam Omar Kumbilamoto alisema serikali ya Samia Suluhu Hassan imewapa kipaumbele watu wenye ulemavu na hivyo Januari hii wanaenda kutoa sh bilioni 14.85 na katika fedha hizi Sh bilioni 2 zinaenda kwa watu wenye uhitaji maalum.
Mbunge wa viti maalum CCM Dodoma Amina Ditopile alimpongeza Steve Nyerere kwa kusaidia wenye ulemavu na kuahidi kuchangia taasisi hiyo sh milioni moja na kuahidi tukio hilo litakapofika Kondoa Mjini basi ataunga mkono kwa asilimia 80.

Mwenyekiti wa Bodi Ofisi ya Hakimiliki Tanzania Cosota Victor Tesha alisema kuna haja ya kuomba taasisi na makampuni mbalimbali nchini wapewe shinikizo la kuajiri walau wenye ulemavu watano kwa kila kampuni moja.
Alisema kila kampuni moja ikifanya hivyo itakuwa imewawezesha kiuchumi kwasababu hawatakuwa ombaomba wengi watajimudu huku akitolea mfano India alienda katika hotel moja na kushuhudia mabubu wakihudumia na wasiokuwa na miguu wakiwa wanapika na hapa nchini inawezekana.
“Tukifanya harambee hatuwezi kuanzisha kiwanda kidogo au hotel kwa ajili ya wenye ulemavu nchini? Tukiwapa ajira ndani ya taasisi zote nchini, Naamini ndani ya miaka mitatu, sio kila mlemavu aliyesoma wengine wanaweza kufanya kazi,”alisema.
Kaimu Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania Dk Gervas Kasiga alisema kwa muda mrefu kulikuwa na filamu zilizotengenezwa kwa maudhui ya walemavu lakini waigizaji wengi hawakuwa wenye ulemavu hivyo wana jukumu la kuwatambua wenye vipaji.
Alisema baada ya kuvutambua watawapa uwezo wa kimasoko na namna ya kukuza kipato kwasababu ulemavu sio mwisho wa kushindwa kufanya vitu na kuahidi kushirikiana na taasisi ya mama Ongea na mwanao kutambua vipaji na kuvipa uwezo wa kuzalisha filamu ili kuwasaidia kiuchumi na kuongeza Pato la Taifa.
“Tunataka kufanya hayo kutafsiri maono ya Rais Samia Suluhu Hassan ambaye hataki kuacha kundi hata moja nyuma, na nyie msijisikie wanyonge tumieni taasisi zenu kuhakikisha mnaweza kujiongezea kipato kupitia taasisi zenu, tumieni vipaji vyenu,”alisema.
Mwisho



