TAASISI za serikali zipatazo 369 zimeunga mkono agizo la Ofisi ya Makamu wa Rais ,Muungano na Mazingira kwa kuacha kutumia nishati ya kuni na mkaa na badala yake kuingia katika matumizi ya nishati safi na salama ya gesi.
Meneja wa mauzo kwa wateja wa Kampuni ya Taifa Gas Tanzania Limited , Moses Massawe amesema hayo Juni 15, 2023 wakati wautoaji mafunzo kwa waandishi wa habari wa Mkoa wa Morogoro kuhusu kampeni ya utunzaji wa mazingira na matumizi ya nishati safi na salama ,tukomeshe uvunaji wa miti kiholela.
Massawe amesema kampuni hiyo inaunga mkono juhudi za serikali katika suala la uhifadhi na utuzaji wa mazingira hivyo imeweka mkakati wa utoaji wa elimu juu ya madhara ya matumizi ya kuni na mkaa.
Amesema kutokana na elimu inayotolewa na kuendelea kutoleaa tayari taasisi 369 za umma imeunganishwa na matumizi ya nishati safi na salama ya gesi.
“ Hadi sasa tumezifikia taasisi 369 za umma ambazo zinatumia nishati safi na salama na katika mkoa wa Morogoro zipo taasisi nane zimeunganishwa na matumizi haya na hivyo zimeondokana na kutumia kuni na mkaa.” amesema Massawe
Massawe amesema katika kukabiliana na changamoto hizo, Taifa Gas kuanzia Julai hadi Disemba mwaka huu imeweka mkakati kuzifikia taasisi 460 na hivyo kufanya jumla ya taasisi 829.
Naye Mkuu wa Chuo cha Ualimu Morogoro , Augustine Sahili ambaye chuo chake limeachana na matumizi ya kuni na mkaa baada ya kuunganishiwa nishati safi na salama (Gas) alisema tabngu kuanza kutumia nishati hiyo wameweza kuokoa milioni 15 kwa mwaka .
“Tunapika chakula kwa muda mfupi na nafuu kuliko mkaa na kuni ambapo kwa mwezi ni Sh milioni 4.5 hadi sh milioni 4.8 na sasa tunatumia Sh milioni tatu kwa matumizi ya gesi na hivyo kuokoa sh milioni 15 kwa mwaka” amesema Sahili
Mei 18, 2018 Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais iliangiza taasisi za serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali na mengine yenye matumizi makubwa ya kuni na mkaa, yatumie nishati mbadala kwa kupikia ikiwa ni njia mojawapo ya kupunguza uharibifu wa mazingira.