MKUU wa Wilaya ya Morogoro, Rebeca Nsemwa amezishauri taasisi zisizo za kiserikali zinazojihusisha na masuala ya usaidizi wa kisheria wilayani humo kufanya utafiti wa kina kubaini kiini cha kukithiri migogoro ya ardhi na kutoa ushauri kwa serikali utaosaidia namna ya kuchukua hatua stahiki.
Nsemwa alisema hayo kwenye hotuba ya uzinduzi wa kampeni ya “Ardhi Yangu, Haki Yangu, Maisha Yangu” ambayo ilisomwa kwa niaba yake na Ofisa Tawala wa Wilaya hiyo,Hilary Sagara.
Uzinduzi wa kampeni hiyo ulimbatana na utolewaji wa mafunzo kwa wasaidizi wa kisheria kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, Gairo, Kilosa, Mvomero na Manispaa ya Morogoro ili kuwajengea uwezo wa mabadiliko ya sheria mbalimbali na kuaminika zaidi kwa jamii katika masuala ya kisheria.
Mkuu wa Wilaya alisema, Mkoa wa Morogoro ni miongoni mwa mkoa yenye migogoro mingi ya ardhi ikiwemo wilaya ya Morogoro ,hivyo taasisi za usaidizi wa kisheria zinapaswa kufanya utafiti wa kina ili kuisaidia serikali kukabilina na migogoro hiyo ya ardhi.
“Natolea mfano kwenye ofisi ya mkuu wa wilaya unapofika ofisini muda wa kuanza kazi unakutana na msululu wa wananchi wanaohitaji huduma lakini wengi wao ni wale wenye migogoro ya ardhi” alisema Nsemwa.
Mkuu wa wilaya alisema, kuwepo wa taasisi ya Liberty Sparks , Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) ,na Shirika la Wasaidizi wa Kisheria Morogoro (MPLC),ni msaada mkubwa wa kutatua migogoro ya ardhi kutokana na kupatiwa ushauri wa kisheria wa kumaliza migogoro hiyo.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Liberty Sparks, Evans Exaud, alisema suala la umiliki wa ardhi kwa wanawake bado ni changamoto kubwa kutokana na kukabiliwa na vikwazo na ubaguzi linapokuja suala la kupata haki na kumiliki ardhi.
Exaud alitaja Changamoto nyingine zinazowakabili wanawake wanapotafuta haki zao ni gharama za mawakili, wengi wao kutokua na elimu ya haki na sheria.
“ Tunahitaji kutoa elimu na kuhamasisha jamii juu ya umuhimu wa haki ya umiliki wa aridhi kwa wanawake na jinsi inavyochangia maendeleo ya jamii na kuhakikisha mila na desturi potofu zinaondolewa na jamii” alisema Exaud
Exaud alisema katika kampeni hiyo miongoni mwa ajenda kubwa ni “ Mazingira Rafiki ya Umilikishaji Ardhi kwa Wanawake : Chachu ya Maendeleo na Suluhusho la Umaskini”.
Naye mmoja wa wasaidizi wa kisheria kutoka wilayani Mvomero, Anna Bahati alisema wao wakiwa ni wasaidizi wa kisheria baada ya kupatiwa elimu , imewasaidia kwenda kuitoa kwa makundi mbalimbali yanayokabiliwa na changamoto ya kudhulumiwa ardhi ,mirathi na kutokomeza mila potofu ndani ya jamii.
Kwa upande wake Ofisa Utawala na Mawasiliano wa MPLC ,Peter Kimath, alisema mila potofu bado zinatumika kwa baadhi ya makabila hasa pale mume anapofariki .
Kimath, alizishauri Taasisi za kisheria na Vyombo vya Habari zinapaswa kuendelea kupaza sauti katika kuwatetea wanawake kwa vile wanazo haki na mali wanazoachiwa na mume baada ya kufariki kwa mujibu wa sheria.
“Tuachane na hizi mila potofu kwamba Baba akifa Mama haruhusiwi kukaa kwenye nyumba au kutumia zile mali zilizopo … elimu zaidi iendelea kutolewa kwa jamii ” alisema Kimath
Comments are closed.