Tabia Bwete chanzo cha magonjwa yasiyoambukiza

Serikali yaelemewa, kutumia mabilioni kutibu

 

MTINDO usiofaa wa maisha kama matumizi ya tumbaku; lishe duni matumizi ya pombe kupita kiasi; kutoshughulisha mwili au kutofanya mazoezi ya viungo mara kwa mara, na unene ukiokithiri vimetajwa kusababisha ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza.

Hayo yamesemwa leo Novemba 11, 2022 na Mkurugenzi wa Tiba kutoka Wizara ya Afya, Profesa Paschal Rugajo katika Kongamano la nne la Kitafiti la Magonjwa Yasiyoambukiza linaloendelea jijini Mwanza.

Amesema utafiti wa mwaka 2018 unaonyesha hapa nchini watu wazima milioni 2.6 sawa na asilimia 8.7 wanatumia tumbaku.

“Utafiti wa mwaka 2012 ulionyesha kuwa matumizi ya pombe kupita kiasi ni asilimia 29.3 na kuna asilimia 34.7 ya watu wana unene uliokithiri.” Amesema

Amesema magonjwa hayo ni mzigo mkubwa kwa serikali kupitia mfuko wa Bima ya afya ambao unalemewa kutokana na magonjwa yasiyoambukiza.

Kwa mujibu wa takwimu za serikali kutoka Wizara ya Afya, gharama za kuhudumia wagonjwa wa saratani wanaopatiwa tiba ya kemikali dawa na mionzi kwa mwaka 2015/16 ni shilingi bilioni 9 na mwaka 2021/22 serikali imelipa shilingi bilioni 22.5

Pia, huduma za matibabu ya figo serikali imetumia shilingi bilioni 9.5 kwa mwaka 2015/2016 lakini kwa mwaka 2021/22 zimetumika Shilingi billioni 35.42.

Idadi ya wagonjwa ni kutoka 280 mwaka huo na kufikia 2099.

“Ukiangalia gharama za matibabu ya moyo zililipwa shilingi milioni 500 kwa mwaka 2015/16 sasa hivi ni shilingi bilioni 4.35 zinatumika.” Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema hivi karibu.

Alisema vipimo vya CT Scan na MRI vimeongezeka kutoka malipo ya Shilingi bilioni 5.43 hadi kufikia Shilingi bilioni 10.89 kwa mwaka 2021/22.

Aidha, Profesa Rugajo amesema inahitajika nguvu ya pamona katika kuzuia vihatarishi ambavyo ni kudhibiti matumizi ya vilevi kama sigara na pombe; kuhamasisha jamii kushiriki mazoezi na kujiepusha na tabiabwete; kuzingatia mlo unaofaa na kanuni bora za lishe pamoja na madhara yatokanayo na uharibifu wa mazingira na tabia nchi.

Nae, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Kasper Mmuya amesema magonjwa yasiyo ya kuambukizwa nchini yanachochewa na tabia bwete ya watu wengi wakiwamo vijana kutoshughulisha miili huku wengi wakiwa hawafanyi mazoezi.

Kwa upande wa Mkurugenzi Msaidizi wa Magonjwa Yasiyoambukiza kutoka Wizara ya Afya, Dk James Kiologwe amesema zaidi ya robo tatu ya wananchi hawajitambui kuwa wana magonjwa yasiyoyakuambukiza na kutaka elimu zaidi itolewe.

Amesema mwanamke mwenye magonjwa yasiyoambukiza yupo katika hatari zaidi ya kujifungua watoto wenye uzito pungufu na pia wapo kwenye hatari zaidi ya kurithisha vizazi vinne, cha kwanza, cha pili, cha tatu na cha nne.

Katika maadhimisho hayo yenye kaulimbiu: ‘Badili Mtindo wa Maisha Boresha Afya.’ Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) ambaye ni Mratibu Wadau Sekta ya Afya, Leticia Rweyemamu, amesema asilimia 74 ya vifo vinavyotokea duniani vinasabishwa na magonjwa yasiyoambukiza.

Kwa mujibu wa Rweyemamu, mwaka 2012 kulikuwa na vifo milioni 157 kati ya hivyo, milioni 41 vilichangiwa na magonjwa yasiyoambukiza. Tangu mwaka 2016 takwimu hizo zimekuwa zikiongezeka na kufikia asilimia 74.

 

Habari Zifananazo

Back to top button