TAFITI: Wafanyakazi baadhi hawana elimu ya kuwekeza

CHAMA cha Wafanyakazi wa Taasisi ya Elimu ya Juu, Sayansi, Teknolojia, Ufundi Stadi, Habari ,Utafiti na Kazi nyinginezo (RAAWU) kimesema tafiti mbalimbali zimeonesha wafanyakazi wengi hawana elimu ya kuwekeza fedha wanapokuwa kazini ili ziwasaidie wanapostaafu kuandisha miradi itakayochangia uendelevu wa kiuchumi.
Mwenyekiti wa RAAWU Tawi la Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Faraja Kamendu amesema hayo kwenye mafunzo kwa waajiriwa na wastaafu watarajiwa waliopo chuo hicho.
Mafunzo hayo ualiandaliwa na RAAWU Makao Makuu kwa kushirikiana na Tawi la SUA ili kuwezesha wafanyakazi kujifunza elimu ya vyama vya wafanyakazi, njia za kusaidia katika ukuaji wa taaluma kazini na maandalizi ya kustaafu.
Pia kuwajengea uwezo utakaosaidia kuyaelewa mazingira yao baada ya kustaafu kwa kuwekeza fedha ili kuepuka changamoto zitakazoweza kuwakabili.
Kamendu amesema utafiti uliofanyika mahala pa kazi umegundua kuna changamoto kwa wafanyakazi wengi ya kukosa elimu ya kutosha juu ya kustaafu waende wakafanye nini na wataishije katika maisha yao mapya hali ambayo inawasababishia wengi wao kupata magonjwa na msongo wa mawazo.
“ RAAWU imemua kufanya mafunzo haya namna ya kuwekeza wanapokuwa kazini na pia mafunzo kwa wastaafu watarajiwa kuwajengea uwezo utakaosaidia kuyaelewa mazingira yao baada ya kustaafu” amesema.
Licha ya hayo aliwasisitiza wafanyakazi kuona umuhimu wa kujiunga na vyama vya wafanyakazi mahala pa kazi ikiwemo RAAWU kwa maslahi yao binafsi na kwa taifa.
Naye Katibu wa RAAWU Mkoa wa Morogoro ,Agnes Gwau amesema uongozi wa chama hicho umeamua kutoa mafunzo hayo ili kuwajengea misingi bora ya kiuwekezaji kwa wafanyakazi.
Amesema kuwa uongozi wa Chama hicho utaendelea kuyaleta mafunzo mara kwa mara ili kuwajenga kiutendaji wanachama wake.
Katika hatua nyingine Menejimenti ya Chuo ya SUA imeipongeza RAAWU kwa kuendelea kuzungumzia na kusimamia maslahi ya haki na wajibu kwa wafanyakazi wa Chuo Kikuu hicho.
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo hicho anayeshughulikia Mipango, Utawala, na Fedha, Profesa Amandus Muhairwa ametoa pongezi hiyo akifungua mafunzo hayo kwa Wanachama RAAWU Tawi la SUA na waajiriwa wapya.
Profesa Muhairwa amewataka wafanyakazi kutekeleza majukumu yao kwa weledi ,kufuata taratibu, kanuni na sheria za utumishi wa umma ili kuchochea maendeleo ya nchi ikiwa na kufikia malengo ya Chuo.



