Tahadhari upepo mkali kuzikumba wilaya 23

MAMLAKA ya Hali ya Hewa nchini imeonya na kuwatahadharisha wananchi katika wilaya 23 juu ya uwezekano wa kuwepo kwa upepo mkali katika kipindi hiki ambacho nchi inaelekea katika msimu wa mvua za masika.
Taarifa iliyotolewa na mamlaka hiyo mwishoni mwa wiki, ilisema upepo huo unatarajiwa kuikumba sehemu kubwa ya nchi hiyo na kwamba unaweza kuendelea hadi Septemba 20 baada ya kuanza tangu Septemba 11.
“Upepo mkali wenye kasi ya kuanzia mita nane hadi 10 kwa sekunde utaendelea katika baadhi ya maeneo ya wilaya za Rutsiro, Karongi, Nyamasheke na Ngororero ikiwa ni sehemu ya jumla ya wilaya 23 zinazotarajiwa kukumbwa na hali hiyo,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Katika baadhi ya wilaya, kasi ya upepo itakuwa mita sita hadi nane kwa sekunde.
Ikitoa mfano, mamlaka hiyo ilisema upepo utapungua kadiri muda utakavyokuwa ukisogea na maeneo mengine hali itakuwa tofauti kabisa.
Ikitoa mfano, taarifa hiyo ilisema: “Kwa mfano, katika wilaya za Kigali, Ngoma, Bugesera, Kamonyi na Gakenke ambako upepo unatarajiwa kufikia kasi ya mita nne hadi sita kwa sekunde.”
Kwa mujibu wa mamlaka hiyo, wakati hali ya upepo ikiwa hivyo, hali ya mvua itakuwa nzuri kwani kutakuwa na mvua kati ya milimita 75 hadi 90 katika siku 10 zijazo hususani katika maeneo ya Rubavu, Nyabihu, Musanze na Burera wakati katika wilaya za Rutsiro, Ngororero, Gakenke, Rulindo, Gicumbi na Rusizi, Nyamasheke na Nyagatare zitakuwa na mvua kuanzia 60 na 75.