TAHEA yahamasisha jamii Iringa kupinga ukatili wa kijinsia

IRINGA: Wakati jitihada za kupinga ukatili wa kijinsia zikiendelea nchini, wadau wa maendeleo wanaendelea kuhamasisha jamii kuongeza uelewa na kuchukua hatua za kukomesha vitendo hivyo vinavyoathiri zaidi wanawake na wasichana.

Katika kuunga mkono juhudi hizo, Shirika la TAHEA Tanzania kupitia Mradi wa REST limeendesha mdahalo wa wazi kwa wananchi wa Kata ya Mseke, Wilaya ya Iringa kuhusu ukatili wa kijinsia na elimu ya afya ya uzazi.
Mdahalo huo umefanyika katika uwanja wa Shule ya Msingi Tanangozi. Hatua hiyo inaendana na juhudi za Tanzania kutekeleza mikataba ya kitaifa na kimataifa ya kulinda haki za wanawake ikiwemo Mkataba wa kutokomeza aina zote za ubaguzi dhidi ya wanawake pamoja na Itifaki ya Maputo ya Umoja wa Afrika.

Akizungumza katika mdahalo huo, Meneja wa Mradi wa REST Wilaya ya Iringa, Hidaya Juma, aliwashukuru wananchi kwa kujitokeza kushiriki kupata elimu kuhusu afya ya uzazi na kupinga ukatili wa kijinsia.
Alieleza kuwa mradi huo unatekelezwa na TAHEA Tanzania chini ya shirika kiongozi DSW Tanzania katika kata nne za Wilaya ya Iringa kwa lengo la kutoa elimu ya afya ya uzazi, kupinga ukatili wa kijinsia na kuwajengea wananchi stadi za maisha.

Kwa upande wake Ofisa Vijana wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Hamis Subuni, alisema mgawanyo sahihi wa majukumu kati ya wanaume na wanawake unaweza kusaidia kupunguza vitendo vya ukatili ndani ya familia na jamii.
Naye Mkuu wa Kituo Kidogo cha Tanangozi kutoka Jeshi la Polisi, Inspekta Joyce Mwamafupa, aliwataka wananchi kutowaficha wahalifu na kutoa taarifa mapema wanapokutana na matukio ya ukatili ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa.

Alisema ushirikiano kati ya wananchi na Jeshi la Polisi ni muhimu katika kudhibiti vitendo vya ukatili wa kijinsia, akiongeza kuwa baadhi ya matukio yameanza kupungua kutokana na kesi kufikishwa mahakamani.
Mdahalo huo umefanyika wakati taifa linaelekea kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani Machi 8, 2026, yenye kauli mbiu: “Haki na Usawa kwa Wanawake na Wasichana ni Msingi wa Maendeleo Jumuishi kuelekea Dira ya 2050.”



