Takukuru ipo tayari ‘mzigoni’ Uchaguzi Mkuu

VITENDO vya rushwa katika uchaguzi ni kati ya vikwazo vya kuwa na uchaguzi unaozingatia misingi ya haki na usawa kwa kuwa vinavyoathiri haki na fursa ya wananchi kuchagua viongozi wanaowataka.

Kuwepo kwa vitendo vya rushwa wakati wa kuchagua viongozi, huwanyima haki wagombea na wananchi. Kutokana na msingi huo na mengine, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU) iko tayari ‘mzigoni’ dhidi ya vitendo vya rushwa kuelekea uchaguzi mkuu huo wa baadaye mwaka huu.

Takukuru chini ya Mkurugenzi Mkuu wake, Crispin Chalamila inatekeleza majukumu yake ya kuufanya uchaguzi ujao usiwe na vitendo vya rushwa kuanzia kwa wananchi wenyewe hadi wagombea. Wiki iliyopita, Takukuru ilifanya warsha kwa makundi mawili muhimu ya wadau wa uchaguzi; vyombo vya habari na vyama vya siasa mkoani Dar es Salaam.

“Tunahimiza wananchi waepuke vitendo vya rushwa na wasikubali kuchagua viongozi wanaotoa rushwa kwa sababu hawana msaada wowote kwao kwa kipindi chote cha miaka mitano ijayo. Hizi ni salamu na ujumbe tunaomba uwafikie wananchi,” anasema Chalamila katika ufunguzi wa mkutano wa wahariri.

Anasema wameanza kutoa warsha kwa wadau ili nao waende kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kufanya uchaguzi kwa umakini kupata viongozi bora wanaowajibika. “Rushwa ni saratani kubwa ambayo haiwezi kukabiliwa na sheria au taasisi moja; ni suala la ushirikishwaji wa wadau wote,” anasema.

Anaongeza: “Tunaamini waandishi wa habari wanaweza kufanya habari za uchunguzi, kufichua vitendo vya rushwa na kusaidia vita ya mapambano na kusaidia jamii isipate viongozi wanaotokana na rushwa.”

Akifungua warsha ya vyama vya siasa, Chalamila anasema ililenga kujadili namna ya kuzuia na kupambana na rushwa katika uchaguzi mkuu huo na kuwajengea viongozi wa vyama vya siasa, uelewa wa kina na uwezo wa kuchukua hatua thabiti kuzuia na kupambana na rushwa katika mchakato wa uchaguzi.

“Lengo hili linazingatia dhana kwamba, vyama vya siasa kama taasisi muhimu katika mfumo wa demokrasia, vina wajibu wa kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa uwazi, uadilifu na ushindani wa haki,” anasema.

Warsha hizo za Takukuru zimekuja wakati mwafaka sahihi kwa kuwa zipo takwimu zinazoonesha kuwapo kwa vitendo vya rushwa wakati wa uchaguzi, lakini pia jamii ina imani na vyombo vya habari, hivyo ni mdau mkubwa katika kuzuia rushwa.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Idara ya Uchunguzi ya Takukuru katika warsha hiyo, malalamiko 647 yalipokelewa katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 na 2020. Kati ya hayo, 588 yalikosa ushahidi, 21 yalifanyiwa uchunguzi na yapo yaliyopelekwa mahakamani na mengine kuchukuliwa hatua za kinidhamu.

Katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024, yalipokelewa malalamiko 135. Miongoni mwa hayo, 87 yalikosa ushahidi na 47 yanaendelea kushughulikiwa katika hatua mbalimbali. Katika mada yake kwa wahariri wa vyombo vya habari, Mkurugenzi wa Uzuiaji Rushwa wa Takukuru, Sabina Seja anasema,

“Takukuru kwa njia mbalimbali ilipokea malalamiko 135 na kufuatilia kwa njia za kiintelijensia matukio 122 kuhusu rushwa au viashiria vya rushwa katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024.”

Anasema malalamiko yalihusu kutoa na kupokea hongo, taratibu za uchaguzi kutozingatiwa, kusafirisha wapigakura, kushawishi wagombea kujitoa, wagombea kutokuwa na sifa na kuruhusu wasio kwenye orodha ya wapigakura kupiga kura.

Anasema malalamiko yalihusu wanachama na mengine 25 yalikuwa dhidi ya wasio wanachama wa vyama vya siasa. Anawataja waliolalamikiwa kuhongwa ni pamoja na wananchi ambao ni wapigakura, makatibu, wajumbe na wanachama ndani ya vyama vya siasa, wenyeviti/ wajumbe wa serikali za mitaa/vijiji na makundi, vijana, wanawake, ‘bodaboda’ na walimu.

Akizungumzia yaliyobainika katika chaguzi zilizopita, Seja anasema katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2014 na 2019, vitendo vya rushwa vilihusisha ugawaji wa fedha taslimu, ugawaji wa vitu kama kanga, fulana, vinywaji na vyakula, ahadi za ajira na mikopo pamoja na upendeleo maalumu kwa wapiga kura endapo wagombea watachaguliwa.

“Mengine yalikuwa kutumia lugha za vitisho, nguvu au mabavu ili kuwalazimisha kupiga kura au kuwazuia wasipige kura,” anasema. Kwa mujibu wa Seja, katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020, vitendo vya rushwa vilikuwa asilimia 72.6 na ugawaji fedha ulikuwa asilimia 64.4.

Anasema rushwa wakati wa uchaguzi si tu ni kosa la kisheria, bali ni ufifishaji wa haki ya msingi ya wananchi kuchagua viongozi wao kwa uhuru. Anasema, “Katika kuhakikisha rushwa haitawali uchaguzi ujao, kila mmoja wetu ana jukumu la kufanya.”

Naye Mkurugenzi wa Elimu kwa Umma Takukuru, Joseph Mwaiselo anasema kuna madhara ya rushwa katika vyombo vya habari wakati wa uchaguzi.

Anayataja baadhi kuwa ni kumnyima haki mgombea au chama cha siasa kuhusu hoja zake kutangazwa au kuandikwa kwenye vyombo vya habari; kuficha uovu wa mgombea au chama cha siasa kujulikana kwa umma; kuandika au kutangaza taarifa za mgombea au chama cha siasa ambazo si sahihi.

Mengine ni kutozingatia misingi ya amani, utulivu, usalama na ulinzi wa nchi wakati wa kutangaza au kuandika habari na kuziwasilisha kwa umma, kutumika vibaya kwa uhuru wa vyombo vya habari, kutokutoa taarifa za tuhuma za rushwa za mgombea au chama cha siasa kwenye vyombo vya habari na Takukuru, na kutokutoa fursa sawa kwa mgombea, chama cha siasa, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) na serikali kwa ujumla.

“Baadhi ya Watanzania wanaamini kuwa, mla rushwa na mbadhirifu wa fedha za umma ni mashujaa. Ili kuondoa mawazo hayo ni wajibu wa vyombo vya habari kushirikiana na Takukuru kuelimisha wananchi kuhusu rushwa na madhara yake,” anasema.

Anaongeza: “Vyombo vya habari ni silaha muhimu dhidi ya rushwa wakati wa uchaguzi kwa kufanya kazi kwa uadilifu na ujasiri. Uchaguzi Mkuu wa 2025 unapaswa kuwa mfano wa demokrasia bora na uwazi.”

Anasema ili kufanikikisha hilo, vyombo vya habari vinatakiwa kuwa mstari wa mbele katika vita dhidi ya rushwa kupitia kuelimisha, kufichua, kushirikiana na Takukuru, kuzingatia na kudumisha maadili na kutoa jukwaa sawa kwa kila chama cha siasa na mgombea.

Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Chalamila anasema rushwa katika uchaguzi ni tishio kwa msingi wa demokrasia kwa kuwa huathiri uamuzi wa wapigakura, huharibu uwazi wa mchakato wa uchaguzi na kuzaa viongozi wasiowajibika.

“Rushwa katika uchaguzi si tu kwamba inapotosha mwelekeo wa uamuzi wa wananchi, bali pia hupunguza imani ya wananchi kwa vyombo vya uchaguzi na serikali kwa ujumla. Mbaya zaidi, hujenga mazingira ya uhasama, migawanyiko ya kijamii na kuvuruga amani ya taifa,” anasema Chalamila.

Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, vyama vya siasa kama wadau wa uchaguzi, vina nafasi ya kipekee katika juhudi za kutokomeza vitendo vya rushwa. “Ndani ya vyama ndipo panapotoka wagombea, hivyo basi mapambano dhidi ya rushwa kwenye uchaguzi hayawezi kufanikiwa pasipo ushiriki wa kweli na wa dhati kutoka katika vyama vyenyewe,” anasema.

Takukuru tayari iko kazini katika suala la rushwa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa baadaye mwaka huu. Kama anavyosema Mkurugenzi wa Elimu kwa Umma wa Takukuru, Mwaiswelo, vyombo vya habari ni silaha muhimu dhidi ya rushwa wakati wa uchaguzi vinapofanya kazi uadilifu na ujasiri.

Habari Zifananazo

One Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button