Takukuru yaitaja Serikali za Mitaa kinara wa rushwa

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani hapa imeitaja Serikali za Mitaa kuwa kinara wa taarifa za rushwa baada ya kubainika kuwa na matukio 35, ikifuatiwa na maendeleo ya jamii ambayo ina taarifa sita.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari jana, Mkuu wa Takukuru mkoani hapa, Sosthenes Kibwengo alisema taarifa hizo sio nzuri hivyo maeneo hayo wanapaswa kuwajibika katika utendaji wao.

Kibwengo alisema tayari wameweka mikakati ya kuhakikisha wanapambana na rushwa katika maeneo hayo zikiwemo sekta binafsi, afya, maji na mahakama ambazo kila moja ilikuwa na taarifa tatu za matukio.

Mbali na hilo, alisema wamefuatilia miradi 31 yenye thamani ya Sh bilioni 19.8 huku ikibaini Wilaya ya Bahi inaongoza watendaji wake kukaa na fedha za makusanyo badala ya kuziwasilisha benki.

Alisema wamekuwa wakiwafuatilia na kuwafikisha mahakamani watendaji ambao wamekula fedha hizo.

Alisisitiza kwamba fedha za makusanyo zinatakiwa zikae ndani ya muda mfupi na baadaye kuwasilishwa benki.

Kibwengo alisema wameanza taratibu za kufuatilia miradi ili kuepusha mianya ya rushwa katika miradi ya maendeleo.

Akizungumzia kuhusu ukatili wa ngono, alisema jamii haipaswi kukaa kimya kwa sababu tatizo hilo ni sugu na linaathiri jamii.

Kutokana na hilo, aliitaka jamii kushirikiana na taasisi hiyo kupambana na rushwa ya ngono vyuoni, shuleni na kazini ambako jamii nyingi inateseka.

Alisema moja ya mikakati ambayo wameweka ni kuhakikisha rushwa inapigwa vita kila mahali na haikubaliki.

Habari Zifananazo

1 Comment
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button