Tamasha la sanaa, utamaduni neema vipato Bagamoyo
WAENDESHA bodaboda, wenye migahawa, hoteli na nyumba za kulala wageni wamesema Tamasha la 41 la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo limewaletea neema kwa kuwaongezea kipato.
Wakizungumza na HabariLEO kwa nyakati tofauti katika siku tatu za tamasha hilo mjini hapa, walisema msimu wa kila mwaka wa tamasha hilo unawapa neema lakini mwaka huu, wamepata zaidi hasa baada ya watu kutoka mataifa mengine kufika kwa wingi na kutembelea vivutio kama Hifadhi ya Taifa ya Saadani na maeneo ya historia ya Kaole.
Mwenyekiti wa waendesha bodaboda Kijiwe Geti Namba 1 Tanesco mjini hapa, Jumanne Hussein alisema tamasha limewanufaisha kibiashara zaidi.
“Mwaka huu tumepata abiria wengi ambao tuliwapeleka Saadani, Msata kijijini na wengine Kaole. Wengine walizunguka kula vyakula vya asili na hawa ni wageni kutoka nje ya nchi,” alisema Hussein.
Alisema kabla ya msimu wa tamasha, walipata kwa siku Sh 15,000 mpaka Sh 20,000 lakini ujio wa tamasha unawawezesha kupata kati ya Sh 50,000 hadi 80,000 kwa siku.
Kauli hiyo ya Hussein insungwa mkono na dereva mwenzake wa pikipiki, Godwin Mushi, aliyesema katika msimu huo wa tamasha alifanya biashara kubwa kiasi cha kubadilisha muda wa kulala kuwa mchana kwa saa chache huku ikimlazimu usiku kukesha.
Mkurugenzi wa New Faith Lodge, James Manyama, alisema tamasha limewaongezea mapato kwani tangu lianze nyumba yake hiyo ya kulala wageni inajaa.
Manyanya anaiomba serikali ikiwezekana ifanye tamasha kama hilo mara mbili mpaka tatu kwa mwaka kwani pamoja na kuwaneemesha kimapato, linakuza mila na tamaduni njema za Kitanzania na kujenga uzalendo
Kuhusu hilo la kukuza utamaduni, Manyanya alipendekeza tamasha liongezwe siku liwe kwa wiki moja kama ilivyokuwa zamani badala ya siku tatu na ushiriki wa makabila yote zaidi ya 120 ya Tanzania uwepo kupitia mila, vyakula, mavazi, nyimbo na ngoma zao ili vizazi vya sasa na wageni kutoka nje waijue zaidi Tanzania.
“Ukweli tamasha hili limetupa neema sana kibiashara, napendekeza lirejeshwe kuwa la wiki na ushiriki wa makabila ya Kitanzania uwe mkubwa zaidi ya sasa tunaona limetawaliwa zaidi na muziki tena wa kizazi kipya bongo fleva na singeli,” alisema Manyama.
Jenifa Kuzoka, mmiliki wa duka la nguo za kiutamaduni na vinyago, alisema wanaishukuru serikali kwa tamasha hili kwani linawapa uhakika wa kipato kwa siku. Anasema ameuza nguo kwa raia wa Zambia waliohudhuria tamasha.
Mama Lishe anayeuza chakula eneo la Stendi ya mabasi Bagamoyo, Mwanahawa Zuberi, alisema tamasha limechangia kuwaongezea mapato na familia zao zina uhakika wa ada, chakula na maisha mengine.
Tamasha la 41 la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni lilifanyika katika Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) kuanzia Novemba 10 hadi jana Novemba 13 likihusisha wasanii wa ndani na nje ya nchi wakiwemo kutoka Zambia, Canada na Kisiwa cha Mayotte.