Tandahimba yakadiria makusanyo ya Bil 40/-

HALMASHAURI ya Wilaya ya Tandahimba mkoani Mtwara imekadiria kukusanya Sh bilioni 40.239 kwa mwaka wa fedha 2025/2026.

Hayo yamejiri leo wakati wa kikao maalum cha baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo kuhusu makisio ya mpango wa bajeti kwa mwaka huo wa fedha 2025/2026, kilichofanyika kwenye halmashauri hiyo.

Advertisement

Akiwasilisha taarifa kuhusu mpango huo wa bajeti, Mkuu wa Idara ya Mipango na Uratibu wilayani humo David Sinyanya amesema bajeti hiyo imezingatia maeneo mbalimbali ikiwemo utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo wilayani humo.

Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Kamishna Msaidizi wa Uhamiaji DCI Mariam Mwanzalima amesema kila mwaka wa fedha wamekuwa na jitihada ya kuhakikisha wanakamilisha miradi ya nyuma ili waweze kwenda na miradi mipya.

Hata hivyo ili waweze kufikia malengo ya makusanyo hayo ni imani yake kwa ushirikiano na wananchi wake wataweza kufikia malengo hayo.

Hata hivyo katika bajeti ya mwaka wa fedha 2024/2025 halmashauri ilikisia kukusanya Sh bilioni 6.1 lakini hadi kufikia Disemba 2024 ilikusanya Sh bilioni 6.9 sawa na asilimia 112.

Mkuu wa Wilaya ya Tandahimba, Kanali Michael Mntenjele kupitia baraza hilo amesisitiza suala la hali ya ulinzi na usalama katika wilaya hiyo kuwa ni salama kwani vikosi vyao vinaendelea na majukumu yake kama kawaida.

“Ila na sisi wananchi tunapaswa kutimiza majukumu yetu ya ulinzi shirikishi ili kuendelea kudumisha hali ya amani katika maeneo yetu”amesema Mntenjele.

Diwani Viti Maalum wilayani humo, Esha Dadi amepongeza bajeti hiyo waliyoipitisha kwenye baraza hilo kwani imegusa maeneo yote muhimu ikiwemo elimu, barabara na mengine.

Katika hatua nyingine kikao hicho kimeridhia kuiunga mkono Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Wilayani humo kwa kuwezesha kiasi cha fedha Sh milioni 6 kwa ajili ya kuwawezesha wakala hao waendelea kuleta ufanisi wa kazi yao hiyo kwenye Wilaya hiyo.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *