Tanesco Kagera watakiwa kutoa elimu vifaa bora vya umeme

MKUU wa Mkoa wa Kagera, Albert Chalamila ametoa wito kwa Shirika la Umeme nchini (Tanesco), mkoani Kagera kushirikiana na taasisi ya udhibiti ubora kuhakikisha wanatoa elimu kwa wafanyabiashra wanaouza vifaa vya umeme, ambavyo vimekuwa vikisababisha hasara kwa wananchi.
Alisema hayo alipofanya kikao na kuzungumza na watumishi wa shirika hilo na kusema baadhi ya wananchi hawana elimu ya kutosha juu ya vifaa mbalimbali vya umeme zikiwemo nyaya na taa.
Alisema umefika wakati wa ushirikiano kati ya Tasisi ya Viwango (TBS) na Tanesco kutoa elimu ya pamoja kuhusu ubora wa bidhaa za umeme, ili kuwaokoa wananchi na hasara, ambazo zinajitokeza mara kwa mara.
“Lazima tujue kuwa hata wafanyabiashara wanaouza vifaa vya umeme, sio wote wenye elimu na wanajua ubora wa bidhaa hizo.
“Ni mara ngapi watumishi wa Tanesco mmeingia madukani kutoa elimu ya vifaa vinavyopaswa kuuzwa kwa wananchi?
Tubadilike na tuchukue hatua, ili kutoa huduma stahiki kwa wananchi wanaotutegemea,”alisema Chalamila.
Kaimu Meneja wa Tanesco Mkoa wa Kagera, Pembe Jeverimo, alisema shirika hilo limeweza kukusanya kiasi cha Sh milioni 134.
9, ambacho kilikuwa kinapotea, lakini baada ya kufungua ofisi ndogo za kuhudumia wateja imeweza kufikisha huduma karibu na wananchi.
Pia alisema uwepo wa ofisi ndogo umesaidia kupunguza malalamiko na kufikisha huduma kwa wananchi, huku wakiwaunganisha wateja wapya 2,406 sawa na asilimia 93 ya malengo yaliyowekwa na shirika hilo kwa mwaka 2021/2022