Tanesco waagizwa kupitia gharama za umeme vijijini

NAIBU Waziri wa Nishati amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji Shirika la Umeme (TANESCO)  Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga kufanya mapitio vijiji vinavyolipishwa kuunganisha umeme kwa bei ya mjini ili kulipa bei stahiki ya vijiji ambayo ni Sh 27,000.

Kapinga ametoa agizo hilo kwa niaba ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko leo bungeni jijini Dodoma, wakati akijibu swali la la Mbunge wa Bukoba Vijijini, Samsung Rweikiza aliyetaka kufahamu mpango wa serikali kwa wananchi wa vijijini wanaolipia gharama ya kuunganishwa umeme zaidi ya 27,000.

Akijibu swali hilo Kapinga amesema: “Kwenye baadhi ya maeneo ambayo ni vijiji na yamekuwa yakitozwa gharama ya Sh 321,000, namuagiza Mkurugenzi Mtendaji Tanesco kufanya mapitio ya maeneo haya.”

Advertisement

Aidha, kuhusu serikali kupeleka umeme vitongoji visivyokuwa na umeme Bukoba Vijijini, Waziri Kapinga amesema serikali inaendelea kuunganisha vitongoji ambavyo havina umeme ambapo vitongoji 258 kati 515 vya Jimbo la Bukoba Vijijjini vimefikishiwa umeme.

Aidha, kazi ya kupeleka umeme katika vitongoji 27 ambavyo havina umeme katika Jimbo la Bukoba Vijijini inaendelea kupitia miradi ya ujazilizi 2B na mradi wa Kupeleka umeme katika vitongoji awamu ya pili A (HEP IIA).

Akijibu swali Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Kilimanjaro, Kunti Msangi aliyetaka kufahamu serikali inafanya jitihada gani kuondoa tatizo la umeme mdogo maeneo ya Kigamboni, Kapinga amesema  serikali inaendelea na maboresho ya kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Mbagala kwa ufungaji wa transfoma yenye ukubwa wa MVA 120 ili kuimarisha upatikanaji wa umeme maeneo ya Kigamboni, Mbagala pamoja na Pwani.

“Transfoma imeshafika na mkandarasi yupo ‘site’ anaendelea na kazi, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge serikali ya awamu ya sita inafanya kila jitihada kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata umeme wa uhakika,” amesema Kapinga.

Akijibu swali la Mbunge wa Nanyumbu, Ally Mhata aliyetaka kufahamu ni lini serikali italipa fidia kwa wananchi wa Wilaya ya Nanyumbu ili kupisha ujenzi wa njia ya umeme ya Grid ya Taifa, Kapinga amesema katika Wilaya ya Nanyumbu, wananchi 689 wanapisha ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa kilovoti 220 kutoka Tunduru hadi Masasi.

Ameongeza kuwa taratibu za kuwalipa fidia wananchi waliopisha mradi zinaendelea ambapo jumla ya Sh billioni 1.95 zinatarajiwa kulipwa kwa wananchi hao