Tangaza nia bila matusi, heshimu kanuni” – MCC Asas aonya wana CCM

IRINGA: MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Salim Faraj Asas, ametoa wito kwa wanachama wa chama hicho wanaotaka kutangaza nia ya kugombea nafasi ubunge na udiwani kufanya hivyo kwa heshima na kuzingatia maadili ya chama.
Aliwahimiza watia nia hao kujieleza kwa hoja na kueleza mipango yao badala ya kutumia fursa hiyo kuwajadili wagombea wengine.
Amesema haipendezi kwa watia nia hao kutumia fursa hiyo kuwachafua, kuwakejeli, kuwatukana na kuwashambulia wanachama wenzao.
Alisisitiza kuwa chama kina taratibu, kanuni na miongozo ambayo kila mwanachama anapaswa kuiheshimu.
SOMA ZAIDI
Kwa mujibu wa Asas, lengo la CCM ni kuhakikisha mchakato wa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2025 unafanyika kwa amani, heshima, na maadili ya kisiasa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Daud Yasin, alisisitiza kutangaza nia si kosa, lakini akasema kufanya hivyo kwa matusi au kuanza kampeni za mapema ni ukiukwaji wa kanuni.
Yasin aliwaonya watia nia dhidi ya kuanza kuzunguka kata au majimbo, akisema huo ni mwanzo wa kampeni kabla ya wakati na kwamba chama hakitasita kuchukua hatua kwa watakaobainika kuvunja taratibu.
Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa Said Goha alisisitiza kwamba CCM itaendelea kusimamia haki, usawa na nidhamu katika mchakato wake wa ndani, huku wakihimiza wanachama kutanguliza maslahi ya chama na taifa badala ya maslahi binafsi.