‘Tangazeni zabuni kwenye mfumo rasmi’

DAR ES SALAAM: Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa 2024, Godfrey Mnzava, ametaka wizara na taasisi zote za serikali kutangaza zabuni za manunuzi ya umma kwenye mfumo rasmi wa kieletroniki, ili kupunguza malalamiko na manung’uniko.

Mwaka 2023 Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), ilianzisha mfumo mpya wa manunuzi wa kieletroniki National e- procurement System of Tanzania (NeST), ili kudhibiti rushwa wakati wa mchakato wa zabuni kuchelewa na kuongeza uwazi wa zabuni.

Mfumo huo ulibuniwa na kutengenezwa na Watanzania na kuanza kufanya kazi Julai Mosi mwaka jana ukichukua nafasi ya mfumo wa awali wa TanNeps uliokoma kufanya kazi Oktoba.

Akizungumza wakati akikagua mradi wa usambazi maji Dar es Salaam ya Kusini (Bangulo), kiongozi huyo amesema mfumo huo utapunguza malalamiko na watu kukutana gizani.

“Mfumo huu unapunguza watu kukutana gizani, waombaji wanaingiza taarifa zao mfumo unachakata, mwenye vigezo anapata bila upendeleo, asiye na vigezo mfumo unamuacha, hii inasaidia kupunguza vitendo vya rushwa,” amesisitiza.

Baada ya kukagua mradi huo wameridhika na kazi inavyoenda pamoja na mchakato mzima uliotumika kumpata mkandarasi.

“Zabuni za manunuzi ya umma ni vyema zitangazwe kwenye mfumo, baada ya ukaguzi tumeridhika ulizingatia mchakato mzima unatakiwa, zabuni zilitaangazwa na mkandarasi ameingia kwenye mfumo, “amesema Mnzava.

Msimamizi wa mradi huo Ishmaeli Kakwezi amesema mradi huo utakapokamilika utawanufaisha wananchi wa Temeke, Ubungo na Ilala.

“Mradi huu ni wa mwaka mmoja umeanza Januari mwaka huu na uatarajiwa kukamilika mwezi Desemba, ambapo utagharimu sh 36 billioni,”amesema Kakwezi.

Amesema tenki hilo litakuwa na mita za ujazo milioni tisa, ambapo wananchi wa Kitunda, Majohe, Kipunguni, Bangulo, Mwanagati na Kivule Kwa upande wa Wilaya ya Ilala, pia utawafikia wananchi wa Ubungo na Temeke

Naye Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu Dawasa, Kiula Kingu amesema tenki kubwa la mradi huo utakua na ujazo wa lita milioni tisa utanufaisha jumla ya kaya 450,000 kutoka majimbo ya Ilala, Ubungo na Temeke.

“Eneo hili lilikuwa na shida kubwa ya maji kutokana na muinuko na hata ukichimba visima ilikuwa ni vigumu kupata maji safi kutokana na kuwa na madini mengi yasiyofaa kwa matumizi ya binadamu,” amesema Kingu.

Kwa upande wa Mbunge wa Ukonga, Jerry Slaa amesema baada ya mradi huo kukamilika utahusisha mtandaao wa usambazaji mji wenye urefu wa kilomita 119 katika jimbo la Ukonga, ambalo limekua na changamoto ya maji.

Habari Zifananazo

Back to top button