Tani 30 mahindi ya msaada zapelekwa Kahama

Tani 30 mahindi ya msaada zapelekwa Kahama

MBUNGE wa Kahama Mjini, mkoani Shinyanga, Jumanne Kishimba amesema zitaletwa  tani 30 za mahindi ya msaada  kutoka Wakala ya  Taifa ya Hifadhi ya Chakula  (NFRA)  na kuwauzia wananchi kwa bei nafuu.

Kishimba alisema hayo jana kwenye mikutano ya hadhara iliyofanyika kwa nyakati tofauti kwenye kata za Malunga  na Mhongolo.

Alisema kilio cha wananchi kimesikika baada ya bei za vyakula kuwa juu  yakiwamo mahindi  hivyo serikali imeona changamoto hiyo na kuitatua kwa kuleta mahindi.

Advertisement

“Tayari mazungumzo yamefanyika na NFRA kwa Kahama Mjini zitaletwa tani 30 za mahindi na kuuzwa kwa bei nafuu,” alisema Kishimba.

Baadhi ya wananchi wa Mjini Kahama,  Joackimu Samweli na Magdalena Issa walisema  changamoto ipo kwenye bei ya vyakula na kuwa debe moja la mahindi wanauziwa Sh 22,000.

Meneja wa NFRA, Kanda ya Shinyanga,  Joseph Maige alikiri tani hizo za mahindi kupelekwa Kahama kuanzia leo ili kupunguza makali ya bei ya mahindi na zitaendelea kupelekwa zaidi ya hizo.

Maige alisema kanda hiyo inajumuisha  mikoa minane ya Kigoma, Kagera, Mara, Simiyu, Geita, Tabora, Mwanza na Shinyanga na  serikali  imejipanga maeneo yote kuwapelekea mahindi hayo na bei elekezi itapangwa.

“Wataendelea kutoa mahindi hayo kwa sababu ya kupanda kwa bei ya mahindi na wananchi wa hali ya chini kushindwa kumudu bei zilizopo sokoni sasa,” alisema.