Tani 3,867 za ufuta zauzwa mnada wa tatu Mamcu

MTWARA: CHAMA Kikuu cha Ushirika cha Masasi Mtwara (MAMCU Ltd) mkoani Mtwara kimeuza tani 3,867 za ufuta kwenye mnada wake wa tatu katika msimu wa mauzo wa mwaka 2025/2026.

Mnada huo umefanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu mkoani humo ambapo bei ya juu ikiwa ni Sh 2,700 na bei ya chini Sh 2,410, uliyoendeshwa kupitia mfumo wa minada wa kieletroniki unaotumiwa na Soko la Bidhaa Tanzania (TMX) kwenye mazao mbalimbali ikiwemo hilo la ufuta.

Akizungumza katika mnada huo, Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu Christopher Magala amewataka wakulima wilayani humo kuendelea kuimarisha na kutunza ubora wa mazao yao mbalimbali yanayozalishwa kwenye wilaya hiyo ikiwemo zao hilo la ufuta ili kukidhi ubora wa soko.

Bashe acharuka mabadiliko vyama vya ushirika

‘’Ndugu zangu wakulima tuelewa kabisa kwamba ubora wa mazao unachangia sana kwenye kupanga bei pia muhimu sana vyama vya msingi kama mnafanya kazi ya kusafisha ufuta iwe ni kabla ya kupima ili kuhakikisha kama uko safi na salama,” amesisitiza Magala.

Mjumbe wa chama kikuu hicho cha MAMCU, Blandina Nakajumo amesema ameviomba vyama vyote vya msingi (Amcos) zinazopokea ufuta zihakikishe zinakuwa na cheke cheke zitazokuwa zinachekecha ufuta kwenye Amcos hizo kinyume na hapo mkulima asikubali kuchukuliwa ufuta wake pasipo kuchekechwa.

Kaimu Mrajisi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Mtwara, Robert Nsunza amesema mnada wa kwanza wa ufuta katika msimu huo wa mauzo wa mwaka 2025/2026 walianza na bei ya juu Sh 2,600  na sasa unapofanyika mnada wa tatu bei ya juu ni Sh 2,700.

“Bei ya ufuta huwa inaanzia juu na kumalizikia juu kutokana na zile nchi zingine zinazozalisha ufuta ikiwemo China yenye uhitaji mkubwa wa ufuta wakati huo inakuwa haizalishi inalima”

Mwakilishi kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA) Agnes Kimaro amesema kinachochangia uwepo wa bei hizo mzuri ni ubora wa mazao ambao unaanzia shambani kwani hawawezi kulima pasipo kufata kanuni za kilimo bora huku akitoa rai kwa wakulima kutumia mbegu bora ili wazalishe mazao yaliyokuwa bora.

Atonene Bakari ni mkulima kutoka Mangaka Amcos, ameishukuru serikali kwa kuendelea kuwaangalia wakulima kwenye suala la bei huku akiwahamasisha wakulima wenzake ambao bado hawajapeleka ufuta ghalani wapeleke ili kuwahi bei mzuri iliyopo sasa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button