“Tani 85,000 za kahawa zinazalishwa kwa mwaka”
BODI ya Kahawa Tanzania (TCB) imesema zao zilo limeendelea kuwa kivutio kikubwa duniani na kwamba kwa sasa uzalishaji wake nchini umefikia tani 85,000 kwa mwaka kutoka tani 50,000.
Hata hivyo imesema ina mpango wa kuendelea kukuza uzalishaji na kufikia tani 300,000 kwa miaka mitano ijayo.
Mkurugenzi wa Masoko TCB, Frank Nyarusi amesema hayo Dar es Salaam katika mkutano ulioandaliwa na Chama cha Kahawa Bora za Afrika (AFCA).
SOMA: Kahawa ya Tanzania kivutio Japan
Amesema zaidi ya wakulima wadogo 320,000 wanategemea kahawa hapa nchini, pia watu milioni mbili wanaitegemea kahawa katika maeneo mbalimbali.
“Kahawa umekuwa kivutio kikubwa duniani inaingiza Dola milioni 200 ni chanzo kikubwa cha mapato katika nchi,” amesema.
Amesema jitihada wanayoifanya ni kushirikisha wadau katika mnyororo wa kahawa, pia kutengeneza mazingira wezeshi ili kila mtu awekeze, auze na kufurahia fursa zote zilizopo kwenye kahawa.
SOMA: Tanzania mwenyeji G25 wazalishaji Kahawa
Mkurugenzi Mtendaji wa TCB, Primus Kimaryo amesema kupitia maonesho hayo wazalishaji, wafanyabiashara na wakaangaji wa kahawa duniani wamealikwa kushiriki kongamano na maonesho ya 21 ya kahawa bora Afrika,.
Kimaryo amesema kongamano hilo linatoa fursa ya pekee kwa nchi ya Tanzania baada ya kufunguka kibiashara.
“Tanzania sasa uzalishaji wetu wa kahawa unaendelea kuongezeka,imekuwa ni fursa kwetu kuona ni namna gani tunaileta tena dunia ya kahawa hapa nchini,” amesema.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya AFCA, Amir Hamza amesema kilichoipa nguvu ya kuleta maonesho hayo Tanzania, ni kutokana na Rais Samia Suluhu Hassan kuifungua nchi kibiashara.