TANZANIA na China zimedhamiria kuendeleza ushirikiano wa kuwanoa wakunga ili wakasaidie kuokoa wanawake wajawazito vijijini kujifungua salama.
Hayo yamesemwa Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Tanzania China Friendship Promotion Association (TCFPA) Joseph Kahama kwenye uzinduzi wa kituo cha mafunzo ya wakunga cha ‘Angel of Life’ .
Amesema ushirikiano katika sekta ya afya ulianza miaka 60 iliyopita ambapo mwaka 1968 China ilileta madaktari na tangu kipindi hicho kumekuwa na mabadilishano ya madaktari wa Tanzania kwenda kusoma China na madaktari wa kule kuja Tanzania kutibu wagonjwa.
“Tunataka kupunguza vifo ya mama na mtoto hasa vijijini ambako kuna umbali mrefu wa kufika zahanati, tumeona wakunga wakipewa mbinu za namna ya kuwaokoa wanawake wajawazito watasaidia maelfu kujifungua salama,”amesema.
Amesema kuzinduliwa kwa kituo hicho kutawezesha baadhi ya wakunga kwenda China kupata mafunzo na Wachina watakuja nchini kuwanoa wakunga wengine ambao hawatapata nafasi ya kwenda.
Katika uzinduzi huo uliohudhuriwa pia, na Makamu Gavana wa Jimbo la Zhejiang kutoka China Yang Qing Jiu ambaye ameahidi kukuza ushirikiano huo na kwamba atatoa nafasi zaidi kuleta wakufunzi kwa ajili ya kutoa elimu kwa wakunga.
Kwa upande wake, Dong Qixin ambaye ni mwakilishi kutoka kampuni ya kimataifa ya Maendeleo na Utamaduni ya Beijing Ambridger Dong Qixin amesema anatamani kuona ushirikiano huo ukiungwa mkono na madaktari mbalimbali wa Tanzania, hospital, wanafunzi na wakunga.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Udaktari cha Wenzhou Chaofun Dong amesema mipango yao ni kuona Tanzania na Afrika inakuwa salama,ana imani ushirikiano huo sio tu, utawanufaisha wakunga pekee bali wagonjwa.