“Tanzania ina nafasi kukuwa kiuchumi 2050”

DAR ES SALAAM: OFISA Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Hanspaul, Satbir Singh Hanspaul amesema kuwa Tanzania ipo katika nafasi nzuri zaidi ya kuendelea ukilinganisha na maono yaliyokuwa kwenye Dira inayoisha muda wake ya mwaka 2002- 2025 na maono yaliyopo kwenye Rasimu ya Dira 2050 ya kufikia pato la mtu kati ya Dola 4700 na 8000 na pato la taifa kufikia zaidi ya Dola bilion 700 ifikapo mwaka 2050.

Ameyasema hayo siku ya Jumatano, Januari 08, 2025 katika Mkutano wa Wafanyabiashara na Wamiliki wa kampuni wa Kuhakiki Rasimu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 uliofanyika katika Serena Hotel, Dar es Salaam.

Amefafanua kuwa matumizi ya mifumo ya kidijiti na Akili Mnemba (AI) yameongezeka maradufu miongoni mwa kampuni, benki na wafanyabiashara hata ambao wapo mbali na miji kitu ambacho hakikuwepo kwa miaka 25 ijayo.

Advertisement

“Kwenye hii rasimu sijaona jambo hili likiangaliwa sana, kwamba sisi kama Watanzania tunatumiaje fursa ya AI?”, amehoji.

Amesema ni muhimu kwa Tanzania pia kujifunza mazuri yanayofanyika kati nchi zingine zilizoendelea kwa kuwezesha Watanzania kuzitembelea nchi hizo kisha kuwarudisha nchini kwa ajili ya kuliendeleza taifa.

“Sisi vijana wetu wengi wanatoka nje ya nchi, wakitoka hawarudi, marafiki wenzangu shuleni tulikwenda nchi fulani, tulikuwa kama 20 lakini tulirudi kama wawili”, ameeleza

Aidha ameeleza kuwa kwenye elimu, kuna umuhimu wa kuwa na mitaala yenye kujumuisha masomo ya uchumi na biashara kwa kiasi kikubwa kwani Watanzania wengi wamekuwa na changamoto ya kushughulika na masuala ya fedha jambo ambalo amesema linalirudisha taifa nyuma.

Katika hatua nyingine, ameipongeza serikali ya Tanzania kwa kutambua umuhimu wa sekta binafsi katika kuchochea maendeleo ya nchi kwa kuweka mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara yanayowafanya kuwekeza zaidi nchini.