Tanzania, India zaahidi kuendeleza ushirikiano

Balozi wa India nchini Tanzania, Binaya Srikanta Pradhan akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella

SERIKALI ya Tanzania na India zitaendelea kuimarisha ushirikiano ikiwemo kuhakikisha sekta za afya na nyingine zinaimarika ikiwemo kilimo.

Akizungumza katika maadhimisho ya miaka 75 ya Jamhuri ya India, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella alisisitiza kwamba Tanzania na India zina ushirikiano wa kihistoria kwenye sekta mbalimbali utakaoendelea kudumu.

Alisema hakuna asiyejua India inavyohakikisha uchumi wao unakua na ndio maana Tanzania inashirikiana nayo katika kuhakikisha maendeleo yanakua kwa kasi ikiwemo kilimo.

Advertisement

“Tuna ushirikiano katika kuhakikisha nchi hizi mbili zinakua kiuchumi, hivyo ushirikiano wa nchi hizi mbili ni muhimu katika kukuza uchumi na kuhakikisha maendeleo yanaimarika,” alisema.

Naye Balozi wa India nchini Tanzania, Binaya Srikanta Pradhan alisema India na Tanzania zina historia katika nyanja mbalimbali ikiwemo kuhakikisha inatoa ufadhili kwa wanafunzi zaidi ya 500 kila mwaka kwa ajili ya kukuza maendeleo.

Alisema nchi hizi pia wanashirikiana na vyuo mbalimbali ikiwemo Taasisi ya Sayansi ya Nelson Mandela katika tafiti za masuala ya maendeleo na kukuza uchumi. Aliahidi kwamba nchi hizo zitaendelea kushirikiana zaidi katika kukuza uchumi na tamaduni mbalimbali.

Awali Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo alishukuru India kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika nyanja mbalimbali ikiwemo sekta ya elimu. Katika maadhimisho hayo Ubalozi wa India ulitoa vitabu kwa baadhi ya shule mkoani Arusha.