Tanzania, Indonesia kushirikiana sekta ya Utalii

DODOMA: Serikali ya Tanzania na Jamhuri ya Indonesia zinajipanga kushirikiana katika masuala ya utangazaji utalii, kubadilishana uzoefu katika masuala ya utalii na ukarimu, tafiti za utalii na kupanua wigo wa mazao ya utalii lengo ikiwa ni kukuza utalii wa nchi zote mbili.

Hayo yamejiri katika kikao kati ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki  na ujumbe kutoka Bunge la Indonesia ukiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Ushirikiano wa Mabunge wa Bunge la Jamhuri ya Indonesia, Fadli Zon kilichofanyika leo Juni 4, 2024 jijini Dodoma.

Akizungumza katika kikao hicho, Waziri Kairuki amesema kuwa Tanzania na Indonesia zinaweza kushirikiana katika kutangaza utalii wao kwa kuunganisha vifurushi vya utalii na kutangaza kwa pamoja nchi hizo mbili ili kuongeza idadi ya watalii.

SOMA: Idadi ya watalii yaongezeka kwa asilimia 96

“Tunawakaribisha baadhi ya wanunuzi kutoka Indonesia ili waweze kuuza vifurushi cha Tanzania na Indonesia na ninaamini tunaweza kufanya kazi kwa pamoja na kuuza vifurushi vyetu kwa pamoja”

Aidha, ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji kutoka nchini Indonesia kuwekeza nchini katika huduma ya malazi kwenye maeneo maalum yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji ndani ya hifadhi na nje ya maeneo ya hifadhi.

Waziri Kairuki ameweka bayana kuwa Tanzania ingependa kujifunza namna ambavyo Indonesia inatangaza utalii wake hasa kwa kutumia teknolojia, mkakati wa kitaifa wa kutangaza utalii, namna ya kutumia mabalozi wa hiari wa utalii na  watu maarufu wenye ushawishi katika jamii, namna ya kutangaza Utalii wa Dini kwa kutumia Mahekalu (temples) na Utalii wa Batik.

Kwa upande wake Dk. Fadli Zon amesema kuwa ushirikiano kati ya Tanzania na Indonesia katika Sekta ya Utalii ni muhimu kwa kuwa nchi hizo mbili zina vivutio vya utalii tofauti.

“Tanzania mna vivutio vya kipekee mfano Mlima Kilimanjaro na  Hifadhi ya Serengeti na wanyamapori watano wakubwa ambao ni kuvutio kikubwa cha utalii (big five) ambao ni Simba, Chui, Tembo, Nyati na Kifaru wakati Indonesia tuna Tembo, Kifaru, Komodo Dragon, Tiger” amesema  Zon.

Pia, amesema Indonesia iko tayari kuutangaza utalii wa Tanzania kwa kutumia watu maarufu wenye ushawishi katika jamii ambao wana idadi kubwa ya wafuatiliaji katika mitandao ya kijamii.

Jamhuri ya Indonesia inakadiriwa kutembelewa na Watalii wa Kimataifa zaidi ya milioni nne kwa mwaka na Watalii wa ndani milioni kumi kwa mwaka.

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button