‘Serikali haijazuia uwindaji wa kitalii’

ARUSHA: Serikali imesema haina mpango wa kusimamisha au kuzuia shughuli za uwindaji wa kitalii na badala yake inaendelea kuandaa na kuboresha sera, sharia na miongozo ili kuzingatia uhifadhi wa wanyamapori, kukuza mapato ya taifa na kuchochea maendeleo ya jamii.

Akizungumza wakati wa kufungua kikao kazi kati ya chama cha wamiliki wa kampuni za uwindaji Tanzania, katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Dk. Hassan Abbas amesema Serikali ya Awamu ya Sita inatambua na kuenzi sekta ya wanyamapori kwakuwa ni rasilimali ya kipekee yenye mchango mkubwa katika uchumi wa taifa.

Ameongeza kuwa ni matarajio ya mkutano huo kuwa utabainisha mikakati ya kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya uwindaji wa kitalii ili kujenga ustawi na kuongeza ushindani wa Tanzania katika soko la uwindaji wa kitalii kimataifa.
Amewataka wadau hao wa uwindaji wa kitalii kuilinda sekta hiyo kwa kuzingatia maadili na kuendeleza uhifadhi na kupmabana na ujangili, kutokukwepa kodi, kulipa kodi na stahiki za jumuiya au wananchi zinazozunguka maeneo ya ya uwindaji.

Akizungumza wakati wa kumkaribisha Katibu Mkuu, Mkurugenzi wa Wanyamapori katika Wizara ya Maliasili na Utalii Dk, Alexander Lobora amesema mikutano ya aina hii imekuwa na tija kwa Serikali na wadau wa tasnia ya uwindaji wa kitalii katika kutafuta suluhu ya changamoto kubwa zinazoikabili tasnia hii.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Kampuni za Uwindaji Tanzania (TAHOA), Michel Mantheakis, ameishukuru Serikali kwa ushirikiano inaoutoa kwa tasnia hiyo na kuongeza kuwa chama hicho kitaendelea kutekeleza wajibu wake kwa kuzingatia sheria na taratibu kwa kuwa kushuka ama kusimama kwa uwindaji wa kitalii.


